Kagilwa atoa maagizo ujenzi sekondari Kiutu

ARUSHA: Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Reuben Kagilwa, ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, Wilaya ya Arumeru, kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya sekondari Kiutu, yanayojengwa kwenye jengo la ghorofa tatu huku ukiwa kwenye hatua ya sakafu ya chini ikiwemo ujenzi wa maabara ya sayansi.
Naibu Waziri Kagilwa ametoa agizo hilo alipotembelea shuleni hapo ili kujionea maendeleo ya shule hiyo mara baada ya shule kufunguliwa na kuanza muhula wa masomo wa mwaka 2026 na kukuta ujenzi wa jengo hilo la ghorofa ukisuasua huku vyumba vya maabara vikiwa bado havijamilika.

Alihoji kwanini halmashauri hiyo imetumia siku nyingi katika ujenzi ilhali wakijua kuwa wanafunzi wanapaswa kutumia maabara kwaajili ya kujifunza kwa vitendo pamoja na madarasa kwaajili ya kuondoa msongamano wa wanafunzi darasani pia aliitaka halmashauri hiyo kuweka vipaumbele muhimu vya utatuzi wa mambo mbalimbali katika maandalizi ya bajeti ya mwaka 2026/27
“Hivi hapa nani anamakosa kwanini wanafunzi wanasoma ila hawana maabara nani amesababisha haya ni wewe mkurugenzi au wewe mtu wa idara ya mipango sasa natoa siku 30 kukamilisha ujenzi wa sakafu ya kwanza ya jengo hili la ghorofa ili kuruhusu wanafunzi kuingia kwenye madarasa hayo na kuanza masomo na mkamilishe maabara za masomo ya sayansi shuleni hapo ambao hazijakamilika kwa muda mrefu sasa
Naye Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dk,Johannes Lukumay ameishukuru serikali kuboresha miundombinu shule ya sekondari Kiutu huku akianisha changamoto kadhaa ikiwemo shule ya sekondari Losinoni ambayo wanafunzi hutembea umbali mrefu wakikabiliwa na hofu ya wanyama wanyamapori huku akiomba shule ya sekondari Olmotonyi kujengwa madarasa manne na bweni moja ili na kupandishwa hadhi kuwa shule ya kidato cha tano na sita.

“Tunashukuru serikali kutoa zaidi ya Sh bilioni 1.7 zilizowekezwa katika ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu, lakini changamoto ya makazi ya walimu bado kubwa mfano shule ya msingi Imayani ambapo walimu husafiri zaidi ya kwenda na kurudi kufundisha”



