Tufanikishe Pamoja wasaidia yatima Temeke

DAR ES SALAAM – KIKUNDI cha kijamii cha Tufanikishe Pamoja kimeungana na uongozi wa Kituo chaThe Valentine Home, kilichopo Kata ya Buza, Wilaya ya Temeke, katika jitihada za kusaidia watoto yatima na wenye uhitaji maalum.
Kituo hicho, kinachoendeshwa chini ya Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam, kinatoa huduma za malezi, ulinzi na mahitaji muhimu kwa watoto wanaotoka katika mazingira magumu ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mwenyekiti wa Tufanikishe Pamoja, Daudi Abdallah, alisema mchango huo ni sehemu ya dhamira ya kikundi kurudisha kwa jamii, huku akisisitiza kuwa jitihada za kuwasaidia watoto zitakuwa endelevu.
“Tunaamini kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila kuwajali watoto walio katika mazingira hatarishi,” alisema Abdallah.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo hicho, Gao John , aliipongeza kikundi hicho kwa mchango wao, akibainisha kuwa msaada huo haukidhi tu mahitaji ya kimwili bali pia huleta faraja na matumaini mapya kwa watoto.

Katika tukio hilo, kikundi kilishiriki katika shughuli za kijamii ikiwemo usafi wa mazingira, kilimo na upandaji wa miti, pamoja na kutoa vyakula, vifaa vya shule na mahitaji mengine ya uendeshaji wa kituo.
The Valentine Home Centre, kilianzishwa mwaka 2015, kinaendelea kutoa huduma kwa watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi katika Temeke na maeneo jirani.
Tufanikishe Pamoja inaitaka jamii kuungana katika jitihada za kuhakikisha ustawi wa watoto yatima unakuwa endelevu, kwani watoto hao ndio msingi wa maendeleo ya baadaye.



