Mchengerwa aonya hujuma Bima ya Afya kwa Wote

WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa ameonya vitendo vya hujuma ndani ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) vinavyoweza kukwamisha mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote (UHI) unaotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Amewataka waandishi wa habari kufanya habari za uchunguzi kufichua vitendo vya udanganyifu na ulaghai katika eneo hilo.

Mchengerwa alieleza hayo wakati wa kikaokazi na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu Bima ya Afya kwa Wote kilichofanyika katika viwanja vya Karimjee mkoani Dar es Salaam.

Mchengerwa alisema katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kuna vikwazo viwili ambayo ni kupambana na magonjwa yanayoweza kuzuiwa kwa kinga, tiba na ubora wa huduma na kingine ni ulaghai na udanganyifu unaoweza kudhibitiwa kwa uwazi, ukaguzi wa mifumo na uandishi wa habari za kiuchunguzi katika sekta ya afya.

“NHIF ikichezewa ikapoteza uaminifu kwa sababu ya ulaghai, wizi na utapeli ambao wengi wetu tanajua yaliyotokea huko nyuma, mifumo itayumba na siko tayari wakati wangu kuona mifumo ikiyumba na kwenye hili nipo tayari kuchukiwa na kila mmoja,” alisema.

Alisema ulaghai ndani ya mifumo ya bima inaweza kusababisha fedha kuanza kuvuja, vituo kucheleweshewa malipo ya huduma, na huduma kuanza kukatika na kusababisha wagonjwa kupata hofu ya gharama za matibabu na kupoteza imani kwa mifumo ya sekta ya afya.

Pia, alisema udanganyifu hufanyika kupitia wagonjwa hewa, madai ya kujirudia, huduma zisizoendana na uhalisia na gharama zisizo na mantiki.

Alisema ulaghai ndani ya bima ya afya si wizi wa fedha peke yake bali ni wizi wa huduma na maisha ya watu na wakichezea mifumo ya bima wanachezea uimara wa taifa.

Alisema serikali itaendela kujenga mifumo imara na kuilinda pamoja na watakaofichua uovu ndani ya sekta ya afya.

Alisema UHI ipimwe kwa uwezo wake wa kudumu na kuhimili mabadiliko ya kiuchumi, idadi ya watu na ongezeko la wagonjwa kupitia mifumo imara na sera bora za sekta ya afya.

“Tutaongeza nguvu kwenye mifumo ya kidijitali, uthibitishaji wa madai na hapa ndipo kwenye changamoto na nyayo za miamala na kanuni zinavyoeleza ili ulaghai upungue kabla haijazaa uovu pili tutaimarisha ukaguzi wa ndani uchambuzi wa data na tutashirikiana na vyombo vya uchunguzi ili udanganyifu usipate nafasi ya kukua,”
alisema.

Alisema wizara haitasita kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kurejesha fedha, kuwawajibisha wanaohusika, kufuta na kuwaondoa watoa huduma wasio waaminifu akiwataka waandishi wa habari kushirikiana kulinda mifumo ya taifa kwa kufanya uandishi wa kichunguzi.

Alieleza ni muhimu rasilimali zitumike kutoa huduma kwa wananchi na si kwenye mifuko ya watu akisisitiza Bima ya Afya kwa Wote italindwa kwa uaminifu na uwazi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button