JKCI yaleta madaktari bingwa kambi ya matibabu Arusha

ARUSHA: MKURUGENZI wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge amesema kuwa mwitikio wa wananchi katika banda lao waliloweka katika kambi ya matibabu Jijini Atusha unaenda vizuri na taasisi hiyo imepeleka madaktari wake bingwa kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu.

Kambi ya matibabu iliyoandaliwa na kuratibiwa na Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Paul Makonda iko katika uwanja wa Shekh Amri Abeid.

Amesema JKCI imepeleka madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo katika kambi ya matibabu jijini Arusha kushiriki na wagonjwa watakaobainika kuhitaji matibabu ya kibingwa au upasuaji wataendelea kuhudumiwa katika taasisi hiyo hata baada ya muda wa kambi kumalizika.

‘’Mtu yoyote atakayegundulika na tatizo la moyo linahitaji matibabu ya kibingwa au hata upasuaji atapokelewa na kupatiwa matibabu na JKCI hata kama muda wa kambi utakapokuwa umekwisha atapewa tiba hadi atakapopata nafuu,”amesema Dk Kisenge.

Dk Kisenge amemshukuru Makonda kwa kuandaa kambi hiyo kwani imeweza kuwasaidia kwa asilimia kubwa wakazi wa Jiji la Arusha, mkoa na nje ya mkoa na kusema kuwa JKCI itakuwa ikishirii kambi hiyo kila mwaka lengo ni kutaka kutoa huduma kwa malengo yaliyokusudiwa na Mbuge wa Jimbo la Arusa Mjini.

Akizungumza katika kambi ya matibabu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Dk Nindwa Maduhu amesema kuwa damu iliyopatikana kwa siku mbili katika kambi hiyo ni unit 50 na mahitaji kwa siku katika hospitali za Jiji la Arusha ni unit 30.

Dk Maduhu amesema mahitaji ya damu katika Jiji la Arusha ni makubwa na ujio wa kambi ya matibabu huenda ikawa suluhisho la changamoto ya damu kwani wengi wamekuwa wakijitokeza kuchangia damu kwa mahitaji ya wagonjwa.

Wakati huo huo gari maalumu la upasuaji lenye teknolojia ya kisasa (Advanced Technology) linalomikiwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili limewasilia jana usiku katika kambi ya matibabu Jijini Arusha lengo ni kutoa huduma za upasuaji katika kambi hiyo ili wananchi wagonjwa wenye uhitaji na huduma ya upasuaji waweze kupata huduma hiyo ipasavyo katika kambi hiyo.

Akizungumzia ujio wa gari hilo la kisasa hapa nchini,Msemaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Irene Mbonde amesema kuwa kuja kwao Jijini Arusha katika kambi ya matibabu ni kufuatia ombi la Paul Makonda na wao wameitikia wito kwa kuwa ni muhimu wao kwenda kutoa huduma ya upasuaji wa aina yote kwa wagonjwa watakaohitaji huduma yao.

Mbonde alisema uwepo wa gari hiyo katika kambi ya matibabu Jijini Arusha ni kupanua wigo wa huduma zinazotolewa na kambi hiyo na kuwawezesha wananchi wa maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha na nje kusogezewa huduma ya upasuaji wa kibingwa karibu.

Wakati huo huo Makonda ameendelea kuwahimiza wakazi wa Jiji la Arusha kuhakikisha wanakwenda kupima afya katika kambi hiyo yenye madaktari wote bingwa hapa nchini na kusema kuwa yeye katika masiaha yake anapenda kuponya na sio kuzika na ndio maana ameratibu na kuanda kambi hiyo ili kutoa huduma za matibabu bure.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button