Nchimbi aongoza mazishi ya Mbunge Munde Tambwe

 MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, leo Februari 4, 2026, ameongoza mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora, Munde Tambwe, yaliyofanyika nyumbani kwao Kata ya Cheyo, Manispaa ya Tabora.

Makamu wa Rais aliongoza mazishi hayo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali, wabunge na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Munde Tambwe alifariki dunia Februari 2, 2026 jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, na kuzikwa katika makaburi ya Sheikh Yahaya yaliyopo Kata ya Kidongo Chekundu mkoani Tabora.

Marehemu alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiiwakilisha Mkoa wa Tabora, nafasi aliyohudumu kwa uaminifu na nidhamu, akijikita katika kuwatumikia wananchi hususan wanawake, vijana na makundi yenye uhitaji maalum. SOMA: Job Ndugai afariki dunia

Katika kipindi cha utumishi wake wa ubunge, alishiriki kikamilifu katika shughuli za Bunge na chama chake, akitetea masuala ya maendeleo ya kijamii, elimu, afya na ustawi wa wanawake, huku akitambulika kama kiongozi mnyenyekevu, mchapakazi na mwenye maadili.

Mbali na siasa, Munde Tambwe alikuwa mshiriki katika shughuli za kijamii na maendeleo katika Mkoa wa Tabora, akichangia juhudi za kuwawezesha wanawake na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button