Watumishi wafundwa mishahara itoshe
WADAU wa uchumi wameshauri watumishi wazingatie mambo matatu ili mishahara yao ikidhi mahitaji na waweke akiba ya baadaye.
Wameshauri watumishi wawe na nidhamu ya fedha, wawekeze kwenye mifuko ya uwekezaji na waepuke mikopo yenye riba kubwa.
“Siku zote mshahara huwa hautoshi, kikubwa ni wewe na bajeti yako unayoishi nayo, hilo ni la kwanza. Kama mimi ninapata mshahara 300,000 (Shilingi) siwezi kwenda kukaa nyumba ya 700,000 nitatafuta chumba cha 15,000 au 20,000,” alisema Rais wa Chama cha Wahasibu, Dk Godvictor Lyimo alipozungumza na gazeti la HabariLEO.
Aliongeza: “Unapozungumzia suala la mshahara kutosha au kutokutosha kwanza tuanze kwa mtu binafsi inawezekana ulipoanza kazi uliiona nyingi inakutosha, baadaye ulipoongezewa uliona aaah! Mbona haitoshi. Hii ndiyo maana halisi ya kusema mshahara huwa hautoshi”.
Dk Lyimo alisema mfumuko wa bei unachangia kufanya mshahara wa mtumishi kutosha au kutotosheleza mahitaji kila siku.
SOMA: Watumishi wa umma washauriwa uwekezaji kabla ya kustaafu
Alihimiza watumishi wazingatie kuwekeza hata kama ni kiasi kidogo kutoka kwenye mishahara yao.
“Watumishi wanatakiwa tuwekeze ndio tutumie na sio kutumia kabla ya kuwekeza, unapata mshahara wa 400,000 (Shilingi), ukatoa mfano 50,000 ukasema hii ni akiba yangu ninaiweka ukawekeza mfano UTT, hii nyingine itakuwa ya matumizi yangu na hakuna hela ndogo hata 10,000 unaweza ukawekeza,” alieleza.
Alisema suala lingine linalochangia watumishi kutojitosheleza na mishahara yao ni wimbi la madeni yasiyomalizika baada ya kukopa mikopo yenye riba kubwa.
“Mikopo ya muda mrefu inawarudisha nyuma, kama mimi mshahara wangu mdogo kwa nini niende kukopa kwenye taasisi ambazo riba zake zipo juu wakati ninaweza nikawa nimejiunga kwenye kikundi cha kuweka na kukopa na nikakopa kwa riba ya asilimia 2 au 3,” alisema Dk Lyimo.
Aliongeza: “Changamoto nyingine ni kutokuwa na subira na mafanikio, unatakiwa kujua kuna baadhi ya vitu ukitaka kuvifanya lazima uweke fedha ndani ya miaka mitano na kuwa na uendelevu wa kuweka akiba ya jambo hilo, lakini ukitaka kwenda haraka ndio unaishia kwenye mikopo”.
Mtaalamu wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Hamphrey Moshi alisema mishahara ya watumishi haijitoshelezi kutokana na gharama za maisha kupanda.
“Serikali inabidi ifanye utafiti wa kuangalia kama mishahara wanayolipa watumishi inawatosheleza au la, na kama haiwatoshelezi basi wanatakiwa kila mwaka wanapopitisha bajeti waangalie namna ya kuongeza mishahara ya watumishi,” alisema Profesa Moshi.
Alisema ni muhimu serikali isimamie ili sarafu ya Tanzania itumike kwenye matumizi ya ununuzi wa bidhaa kimataifa ili bidhaa zisipande bei kutokana na kupanda kwa thamani ya fedha za kigeni.
“Itasaidia kushusha mfumuko wa bei kwa kiasi kikubwa na tutumie kilimo kukuza mahitaji ya chakula nchini ili kiwe kingi watumishi na watu wengine wapate kwa bei rahisi,” alisema Profesa Moshi.
Alisema watumishi wanatakiwa kuwa na nidhamu kwenye matumizi ya fedha ili waweze kufikia malengo yao.
“Nidhamu ya fedha ndio itaweza kuuokoa mshahara wa mtumishi na uweze kuwa na tija kwenye maisha yake, asipokuwa na nidhamu ya fedha hata apewe kiasi gani hautatosha,” alisema Profesa Moshi.
Mtaalamu wa uchumi, Jeremiah Mwakasita alihimiza watumishi wawe na nidhamu katika matumizi ya fedha ili kujiandaa kwa maisha baada ya utumishi.
Miezi kadhaa iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema wataalamu walikaa wakajiuliza ikiwa watu walipwe kwa wingi wa majukumu au kigezo cha elimu, lakini walielekeza kuwa elimu na ujuzi ndicho kiwe kigezo cha kutofautisha mishahara kwa mtu mmoja na mwingine.
Chalamila alisema Dar es Salaam mshahara unaanza kutofautiana na kuonekana hautoshi wakati majukumu yanabadilika na kuongezeka.
“Mshahara huwa ni kianzio kisichogawika ili kigawike lazima tena uhame kutoka kwenye kila kisichogawika kukiunda vizuri ili kiwe sehemu ya faida utakayotumia kuigawa kwa wake walioongezeka, ukibaki kuilalamikia serikali na kukata tamaa juu ya unachokipata utakuwa si balozi mzuri,” alisema Chalamila.



