Vijana Kagera wapewa elimu mikopo ya halmashauri

KAGERA: Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM, (UV CCM) mkoani Kagera imezindua kampeini ijulikanayo kama Vijana Daka Fursa na Samia maarufu kama VIDAFUSA ambayo imeenda sambamba na utaoji wa elimu ya namna bora ya kutumia mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na halmshauri kwa makundi maalumu.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Faris Buruhani, amesema zaidi ya Sh bilioni 1 zimetolewa kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, hatua iliyochochea kuinuka kwa vijana kiuchumi katika mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari Buruhani alisema utekelezaji wa kampeini maalum ya Vijana Daka Fursa na Samia, iliyofanyika katika halmashauri zote nane za Mkoa wa Kagera kwa lengo la kuhamasisha vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan umefanikiwa navijana ambao tayari wamepata fedha hizo na ambao hawajapata wamefikiwa na elimu hiyo.

Amesema kuwa kampeini hiyo kupitia , UVCCM imetoa elimu kwa vijana kuhusu namna ya kuunda vikundi vya uzalishaji mali, kuandaa maandiko ya miradi yenye tija na kufuata taratibu sahihi za kuomba mikopo ya asilimia 10 inayotengwa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa Buruhani, jumla ya vikundi 59 vya vijana vimefanikiwa kunufaika na mikopo hiyo, fedha ambazo zimewekezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi, biashara ndogo ndogo na utoaji wa huduma.

Amesema vijana wengi wanapaswa kujengewa uwezo wa kujitegemea.
Amesisitiza kuwa bado kuna haja ya kuongeza elimu kwa vijana kuhusu fursa zilizopo ili kuhakikisha hakuna anayekosa mikopo hiyo kutokana na ukosefu wa taarifa au urasimu usio wa lazima.

Aidha, amewataka Maafisa Maendeleo katika halmashauri zote kutoka maofisini na kuwafikia vijana moja kwa moja, ili kuwasaidia kuandaa miradi bora na kusimamia ipasavyo mikopo wanayoipata.

Amesema kuwa UVCCM itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mikopo hiyo ili kuhakikisha inarejeshwa kwa wakati na kuwafikia vijana wengi zaidi, akisisitiza kuwa vijana wa Kagera wana uwezo wa kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button