Wahariri wakutana na Tume ya uchunguzi

TUME ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, leo Machi 3, 2026 imekutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini.
Mkutano huo wa Tume na wahariri umefanyika katika Ukumbi wa Kilimanjaro uliopo katika jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mkoani Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tume kukusanya taarifa, maoni na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu, wananchi, pamoja na viongozi wa sasa na waliostaafu.SOMA: Tume ya uchunguzi yakutana na Abdurahman Kinana

Katika mkutano huo, hoja zilizojadiliwa zilihusu chanzo na tathmini ya athari za matukio hayo ndani na nje ya nchi, pamoja na ushauri wa hatua za kijamii na kisheria zinazoweza kuchukuliwa ili kuimarisha amani, mshikamano wa kitaifa na kuhakikisha matukio hayo hayajirudii tena.
Tume inaendelea na mahojiano na waathirika wa matukio hayo, baada ya hivi karibuni Mamlaka ya Uteuzi kuiongezea muda wa siku arobaini na mbili (42) kuanzia Februari 20, 2026 ili iweze kukamilisha uchunguzi huo. Tume imeelekezwa kukamilisha kazi yake na kuwasilisha taarifa kabla au ifikapo Aprili 3, 2026.



