RC Iringa azindua wiki ya utafiti na bunifu

IRINGA: Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amefungua rasmi Wiki ya Utafiti, Ubunifu na Huduma kwa Jamii iliyoandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), akisisitiza umuhimu wa tafiti na ubunifu katika kutatua changamoto za wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi.
Maadhimisho hayo yanayofanyika kuanzia Juni 2 hadi 4, 2026 katika Viwanja vya Bustani ya Manispaa ya Iringa, yamewakutanisha taasisi za elimu ya juu, taasisi za utafiti, sekta binafsi na taasisi za umma kuonesha tafiti, bunifu na huduma mbalimbali kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Kheri alisema mfumo wa kuwakutanisha wadau wote katika eneo moja unarahisisha wananchi kupata huduma na taarifa kutoka taasisi mbalimbali kwa wakati mmoja kupitia mfumo wa One Stop Centre.
Alisema utaratibu huo unatoa nafasi sawa kwa taasisi kubwa na ndogo kuonesha mchango wao katika maendeleo ya jamii huku ukiongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali.

“Mwananchi anapokuja hapa anakutana na taasisi zote katika eneo moja. Hii ni hatua muhimu inayorahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu ya taasisi mbalimbali,” alisema Kheri.
Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza kuwa tafiti zinapaswa kuwa msingi wa maamuzi ya viongozi na taasisi, akieleza kuwa maendeleo endelevu yanahitaji ushauri unaotokana na ushahidi wa kisayansi.
Alisema utafiti bora una mchango mkubwa katika kusaidia serikali na wadau wa maendeleo kubaini suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta mbalimbali.

Katika maonesho hayo, Kheri alipongeza watafiti na wabunifu kwa kuendelea kubuni teknolojia na bidhaa zinazotumia rasilimali zilizopo ndani ya nchi, akitolea mfano tafiti zinazohusu matumizi ya zao la ulanzi katika kutengeneza bidhaa za kitabibu na viwandani.
Alisema ubunifu huo unaweza kusaidia kuongeza thamani ya mazao ya ndani, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kufungua fursa mpya za ajira na uwekezaji.

Kwa lengo la kuimarisha maadhimisho hayo, Kheri alitangaza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa itatoa Sh Milioni 20 kama mchango wa kuanzia maandalizi ya Wiki ya Utafiti, Ubunifu na Huduma kwa Jamii ya mwaka 2027.
“Tunataka maonesho haya yawe makubwa zaidi kila mwaka na kuifanya Iringa kuwa kitovu cha utafiti, ubunifu na utoaji wa huduma kwa jamii katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,” alisema.
Kwa upande wake, Rasi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Profesa Method Samuel Semiono, alisema chuo hicho kinaendelea kuwekeza katika tafiti na bunifu zinazolenga kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo mkoani Iringa na nchini kwa ujumla.
Alitaja baadhi ya miradi inayooneshwa katika maadhimisho hayo kuwa ni uzalishaji wa ethanol kutoka kwenye ulanzi, uzalishaji wa uyoga wenye virutubisho maalumu pamoja na utafiti wa kemikali za kudhibiti mdudu waharibifu wa zao la nyanya anayejulikana kama Kantangaze.
Profesa Semiono alisema MUCE imetenga zaidi ya Sh Milioni 300 kusaidia maendeleo ya bunifu hizo ili zifikie hatua ya uzalishaji wa kibiashara na kuwanufaisha wananchi pamoja na sekta ya viwanda.
Aliwahimiza wadau wa maendeleo, wawekezaji na sekta binafsi kushirikiana na vyuo vikuu katika kuendeleza matokeo ya tafiti ili yaweze kugeuzwa kuwa bidhaa na huduma zenye tija kwa jamii.



