Wizara ya Kilimo, taasisi zashiriki maonesho Siku ya Mazingira Duniani

DODOMA: Wizara ya Kilimo pamoja na taasisi zake zimeendelea kushiriki Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyoanza jijini Dodoma mnamo Juni Mosi na kutarajiwa kufungwa rasmi Juni 6, mwaka huu.

Lengo la maonesho hayo ni kuonesha  malengo ya maonesho hayo ni kuonesha mchango wa sekta ya kilimo katika uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika maonesho hayo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), zimeonesha teknolojia mbalimbali zinazochangia kuongeza uzalishaji wa kilimo sambamba na utunzaji wa mazingira.

Akitoa maelezo kwa viongozi na wadau mbalimbali waliotembelea banda la Wizara ya Kilimo katika maonesho hayo, ofisa Mazingira wa Wizara ya Kilimo, Omary Abdallah amesema kuwa Wizara imeendelea kuwekeza katika tafiti za kilimo, ikiwemo uendelezaji wa mbegu himilivu kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

Miongoni mwa viongozi waliotembelea banda hilo na kupatiwa maelezo juu ya sekta ya kilimo ni pamoja na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Switbert Zacharia Mkama.

Aidha, amebainisha kuwa Wizara imetekeleza na inaendelea kutekeleza Mpango wa Sekta ya Kilimo wa Usimamizi na Utunzaji wa Mazingira (ASEAP) pamoja na Mpango wa Sekta wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa lengo la kuimarisha ustahimilivu wa sekta ya kilimo dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Naye ofisa Kilimo Mkuu kutoka Idara ya Maendeleo ya Mazao, Sehemu ya Huduma za Ugani, Zainabu Mchomvu alieleza kuwa Wizara imeendelea kuimarisha huduma za ugani kwa kushirikiana na TAMISEMI pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuwafikishia wakulima elimu na mbinu bora za kilimo rafiki kwa mazingira.

Ameeleza kuwa juhudi hizo zimechangia kuongeza uzalishaji wa mazao, kuhifadhi mazingira na kuimarisha uwezo wa wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo kuendeleza kilimo chenye tija na endelevu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button