Mkakati maalumu kudhibiti bidhaa za magendo

TANGA: Ili kudhibiti uingizwaji wa bidhaa za magendo katika mpaka wa Horohoro, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Serikali imetangaza operesheni kabambe ya kusambaratisha magendo na biashara haramu zinazotishia usalama wa taifa na kupoteza mapato ya Serikali.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, wakati wa ziara yake katika Kituo cha Forodha cha Horohoro, ambako amesisitiza kuwa Serikali haitafumbia macho mtandao wowote wa uvunjifu wa sheria mipakani.

Balozi Omar alionya kuwa biashara ya magendo ni tishio kwa usalama wa nchi, akibainisha kuwa jukumu la maofisa forodha na vyombo vya ulinzi si kukusanya mapato pekee, bali ni kuhakikisha bidhaa hatarishi hazipenyezwi nchini.
“Tusipotekeleza jukumu hili ipasavyo, tutalisababishia Taifa madhara makubwa. Usalama wa Taifa ni jambo ambalo hatuwezi kulifumbia macho hata kidogo,” alisisitiza Balozi Omar.
Aliongeza kuwa ukusanyaji wa takwimu sahihi za biashara ni nyenzo muhimu kwa Serikali katika kupanga mipango ya maendeleo, hivyo magendo yakistawi, uchumi wa taifa unakuwa hatarini.

Naye Ofisa Mfawidhi wa Kituo cha Forodha Horohoro, Shadrack Mbonea, alieleza kuwa kukosekana kwa mashine ya kisasa ya kukagua mizigo (Scanner) kinafanya kazi kuwa ngumu.
Aidha, tatizo sugu la kukatika kwa umeme mara kwa mara kutokana na uchakavu wa miundombinu, jambo linalotajwa kukwamisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima, alisema kuwa miundombinu mibovu ya barabara za mpakani ndiyo inayotoa mwanya kwa wahalifu kutumia ‘njia za panya’ kukwepa forodha.



