Miradi ya Sh bilioni 23.6 yafungua fursa Mufindi

IRINGA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) imeendelea kuthibitisha utekelezaji wa ahadi zake kwa vitendo baada ya Kamati ya Siasa ya Chama hicho Mkoa wa Iringa kujiridhisha na utekelezaji wa miradi miwili mikubwa ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 23.6 katika Wilaya ya Mufindi, ambayo imeboresha huduma za afya na kufungua fursa mpya za ukuaji wa uchumi kwa wananchi

Kamati hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, ilikagua ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Mtiri–Ifwagi yenye urefu wa kilomita 14 iliyogharimu Sh bilioni 21.9 pamoja na mradi wa mtambo wa kisasa wa kuzalisha oksijeni tiba katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mafinga uliogharimu Sh bilioni 1.78.

Akiwasilisha taarifa ya mradi wa barabara, Meneja wa TARURA Mkoa wa Iringa, Mhandisi Davies Tembo, alisema mradi huo ulitekelezwa chini ya Programu ya RISE (Roads to Inclusion and Socioeconomic Opportunities) inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wizara ya Ujenzi.

Alisema ujenzi ulianza Julai 27, 2023 na kukamilika Desemba 28, 2024, huku kipindi cha uangalizi wa mkandarasi kikihitimishwa Juni 30 mwaka huu.

Mhandisi Tembo alisema kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kukata milima, kupasua miamba, kujenga madaraja mawili, makalavati 37, kuweka tabaka mbalimbali za barabara pamoja na kufunga taa 90 za barabarani.

Pia maeneo yenye miteremko mikali yalijengwa kwa zege ili kuongeza uimara wa miundombinu hiyo.

Alieleza kuwa barabara hiyo imeondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi wa Ifwagi na maeneo jirani, kurahisisha usafirishaji wa mazao ya misitu, chai, mboga mboga na mazao mengine ya biashara, huku ikipunguza gharama za usafiri na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na utawala.

Kamati hiyo pia ilikagua mradi wa mtambo wa kuzalisha oksijeni tiba katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mafinga, ambao umejengwa kwa ushirikiano wa Serikali Kuu na Global Fund kwa zaidi ya Sh bilioni 1.7.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Dk Bonaventura Chitopela, alisema mtambo huo wenye uwezo wa kuzalisha mitungi 60 ya oksijeni yenye ujazo wa lita 100 kwa siku umeongeza ubora wa huduma za dharura, wagonjwa wa chumba cha uangalizi maalumu (ICU), watoto wachanga na wajawazito.

Alisema kabla ya mradi huo hospitali ilikuwa ikitumia wastani wa Sh milioni 9 kila mwezi kununua oksijeni, lakini gharama hizo zimepungua hadi Sh Milioni nne, hivyo kuokoa takribani Sh milioni 5 kila mwezi ambazo sasa zinaelekezwa kuboresha huduma nyingine za afya.

Aidha, alisema mtambo huo hauhudumii hospitali ya Mafinga pekee bali pia unasambaza oksijeni tiba katika hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, hospitali ya Manispaa ya Iringa, hospitali ya Rufaa ya Ipamba pamoja na vituo vingine vya kutolea huduma za afya.

Baada ya kukagua miradi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, alisema Kamati ya Siasa imeridhishwa na ubora wa utekelezaji wake pamoja na manufaa makubwa yanayoendelea kupatikana kwa wananchi.

Alisema barabara ya Mtiri–Ifwagi imefungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi kwa kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, huku mtambo wa oksijeni ukiwa suluhisho la kudumu la upatikanaji wa huduma muhimu za afya na kupunguza gharama za uendeshaji wa hospitali.

“Miradi hii ni ushahidi kwamba CCM inapowaahidi wananchi, Serikali inayoiunda hutekeleza kwa vitendo. Haya ndiyo matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo wananchi wa Mufindi wanayaona na kuyafaidi,” alisema Yassin.

Aliwataka wananchi kuitunza miundombinu hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ifwagi, Arafat Benson Mwambule, alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha za ujenzi wa barabara hiyo, akisema tayari imechochea shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa wananchi, huku wakisubiri utekelezaji wa awamu zinazofuata za ujenzi.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ifwagi, Fransis Bilangulo, alisema barabara hiyo imeibadilisha sura ya kijiji na kuongeza kasi ya shughuli za kiuchumi, jambo lililoifanya Ifwagi kuwa miongoni mwa maeneo yaliyonufaika zaidi na uwekezaji wa Serikali katika miundombinu.

Ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa ni sehemu ya ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM na tathmini ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za umma, ikiwa na lengo la kuhakikisha ahadi zinazotolewa kwa wananchi zinatekelezwa na kuleta matokeo yanayogusa maisha yao moja kwa moja.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button