Maofisa elimu kuwezeshwa mikopo

ARUSHA: BENKI ya CRDB imesaini mkataba wa miaka mitano na Umoja wa Maofisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania Bara (REDEOA) kwa lengo la kutoa mikopo wezeshi, mafunzo ya ujasiriamali na huduma za kifedha zitakazowawezesha maofisa elimu kujikwamua kiuchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa alisema ushirikiano huo ni muhimu kwa kada ya maofisa elimu kwani utawafungulia fursa mbalimbali za kiuchumi.

Amesema kupitia makubaliano hayo, benki hiyo itatoa elimu ya fedha, ujasiriamali na usimamizi wa mitaji, sambamba na kuwafundisha walimu kuhusu akiba, uwekezaji na matumizi sahihi ya mikopo
Mbali na huduma za kifedha, benki hiyo imekuwa ikishiriki katika shughuli za kijamii zikiwemo ujenzi wa viwanja vya michezo, ugawaji wa madawati, ujenzi wa shule, upandaji miti na uchimbaji wa visima ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Mkurugenzi wa Elimu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dk, Emmanuel Shindika, ameishukuru benki hiyo kwa kuwaona walimu kama kundi muhimu linalostahili kupewa fursa za kiuchumi kupitia mikopo mbalimbali na kujikita katika kilimo ili waone fursa za maisha kupitia ualimu.



