Takukuru yasaidia TRA kuokoa Sh mil 57

KAGERA: TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesaidia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya zaidi ya Sh milioni 57 kutoka kwa wafanyabaishara waliokwepa kodi na kuingiza bidhaa bila vibali.
Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Vangisada Mkalimoto ametoa kauli hiyo leo Machi 4, alipotoa taarifa ya utenda kazi wa taasisi hiyo kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka 2025.
Katika msako huo, magari matano yalikamatwa yaliyosheheni bidhaa mbalimbali zikiwemo tani 38, tani 16 na tani 33 za karanga, injini ya gari pamoja na katoni 303 za pombe haramu. Magari hayo yalikuwa yakitumia njia zisizo rasmi kupitisha mizigo hiyo nchini.
Kamanda huyo amewaonya watumishi waliopo katika mipaka kufanya kazi kwa weledi na uaminifu na kuongeza kuwa hatua stahiki zinachukuliwa kwa mtumishi yoyote atakayeshindwa kutimiza wajibu wake.
“Tumeongeza mafunzo mpakani kwenye vituo vya forodha juu ya kutambua wakwepa kodi ,lakini hatujasahau ufatiliaji kwa watumishi wa mpakani ikiwa mtumishi atahusika moja kwa moja kukwepa kodi lazima achukuliwe hatua za kisheria kwa hiyo watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa weledi,”alisema Mkalimoto.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU mkoani humo imepokea jumla ya malalamiko 121 yanayohusiana na tuhuma za rushwa katika kipindi hicho. Kati ya hayo, malalamiko 86 yalihusu rushwa, ambapo baadhi ya kesi zimefunguliwa mahakamani na nyingine zinaendelea kuchunguzwa.
Aidha, taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa kupitia mikutano ya hadhara, semina na klabu za wapinga rushwa, ambapo zaidi ya wananchi 19,250 wamefikiwa.
TAKUKURU imewataka wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na magendo ili kulinda uchumi wa nchi na kuimarisha utawala bora.



