Serikali yaitaka MUHAS kujizatiti tafiti magonjwa adimu

DAR ES SALAAM: Serikali imewataka wataalamu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kujizatiti kusoma na kufanya tafiti za kina kuhusu magonjwa adimu ili kusaidia kubaini chanzo chake, njia za matibabu na namna ya kuyadhibiti kwa ufanisi nchini.

Hatua hiyo itaimarisha mifumo ya huduma za afya kupitia tafiti ili kuhakikisha wagonjwa wenye magonjwa adimu wanapata huduma stahiki kwa wakati.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe ametoa rai hiyo Machi 4 wakati akifungua Kongamano la 16 la kusambaza matokeo ya tafiti za magonjwa adimu lililofanyika chuoni hapo jijini Dar es Salaam.

“Serikali inayapa uzito stahiki magonjwa haya adimu, ili tuweze kuyashughulikia kwa kina na upana wake, kwa kushirikiana na Taasisi kama Ali Kimara, sekta mashirika na sekta binafsi tutawafikia watoto wengi zaidi,” alisema Dk Magembe.

Aidha, Dk Magembe amesema hadi kufikia Desemba mwaka 2025 zaidi ya wataalamu wa afya 200 katika vituo 14 walikuwa wamepatiwa mafunzo ya kuanzisha vitengo vya tiba ya magonjwa adimu ikiwemo ‘hemofilia’ kuanzia ngazi ya msingi.

“Serikali imeshachukua hatua za kujenga uwezo wa maabara yetu ya taifa, mafunzo kwa wataalamu wa afya na kuanzisha vitengo maalumu vya matibabu ya magonjwa adimu kuanzia ngazi ya msingi zahanati, kituo cha afya na hospitali za wilaya,” alisema Dk Magembe.

Kongamano hilo limewakutanisha wataalamu wa afya, watafiti, watunga sera, wawakilishi wa wagonjwa pamoja na wadau mbalimbali kujadili changamoto na fursa zilizopo katika kushughulikia magonjwa adimu nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya alisema kongamano hilo linalolenga kuimarisha mjadala, kubadilishana uzoefu na kuibua mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utambuzi, matibabu na ubora wa maisha ya wagonjwa.

Aliongeza kuwa chuo hicho kina wajibu wa kuendeleza elimu, tafiti na ubunifu katika eneo la magonjwa adimu, hasa ikizingatiwa changamoto ya upatikanaji mdogo wa vipimo vya vinasaba na gharama kubwa za uchunguzi.

Aidha, katika kuunga mkono juhudi za utafiti na uelimishaji kuhusu magonjwa adimu, Ali Kimara Rare Diseases Foundation walitoa msaada wa fedha kwa ajili ya kusaidia kufanikisha tafiti zinazohusu masuala ya magonjwa adimu.

Kongamano hilo limeandaliwa na MUHAS kwa kushirikiana na Taasisi ya Ali Kimara Rare Disease Foundation (AKRDF).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button