Migogoro 60 yapatiwa ufumbuzi Samia Ardhi Kliniki

KIGOMA: MIGOGORO 60 ya Ardhi imetatuliwa katika siku tatu za mpango wa kusikiliza malalamiko ya ardhi maarufu kama ‘Samia Ardhi Kliniki’ katika Manispaa ya Kigoma Ujiji ikiwani sehemu ya maadhimisho kuekelea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani.
Mkuu wa Wilaya Kigoma, Dk Rashid Chuachua amesema hayo katika uwanja wa Kawawa Ujiji Mjini Kigoma ambako kliniki hiyo inaendelea na kueleza kuwa tangu Machi 2 kliniki hiyo ilipoanza jumla ya migogoro 90 ilikuwa imepokelewa na kusikilizwa.

Dk. Chuachua alisema kuwa ipo migogoro ya ya mirathi na mipaka iliyochukua muda mrefu ambayo ilimalizwa kwa watu wanaogombana kukubaliana baada ya mazungumzo yaliyosimamiwa na mkuu huyo wa wilaya na hivyo wataalamu kwenda eneo la tukio kubainisha mwisho wa mipaka ya kila mmoja.
Alisema baada ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika Machi 7, kliniki hiyo itaendelea kwa ngazi ya wilaya hadi Machi 16, ikihusisha kata na vijiji mbalimbali vya Halmashauri ya Wilaya Kigoma na Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Ofisa Ardhi Mteule wa Mkoa Kigoma, Elias Mwazembe alisema kuwa sehemu kubwa ya migogoro hiyo ni uelewa wa mambo ya wananchi kwani ipo migogoro ya ardhi ya masuala ya mirathi ambayo ipo mahakamani hivyo wao wanawaelekeza wahusika kuendelea na kesi zao mahakamani lakini wamekuwa wakitoa ushauri kwa mahakama uhalisia wa kupatia ufumbuzi wa migogoro hiyo.
Mwazembe alisema kuwa mingi ya migogoro ya mirathi kwenye ardhi inakuja kwenye suala la baadhi ya ndugu kutaka kuuza mali hizo huku baadhi ya ndugu wakitengwa kwwenye umiliki hivyo suala hilo huwa linarudishwa mahakamani ili sheria ya mirathi iweze kutekelezwa katika mgawanyo wa mali.



