Mkandarasi kiwanda cha TSN aongezewa miezi 3

MKANDARASI anayejenga Kiwanda cha Uchapaji cha Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ameongezewa miezi mitatu akamilishe kazi hiyo. Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema hayo  alipotembelea mradi huo uliopo Makao Makuu ya TSN, Tazara katika Barabara ya Mandela, Dar es Salaam jana.

“Mkandarasi amepewa miezi mitatu mingine ambayo inaanza siku ya kesho (leo) ambayo itakuwa inaisha Juni 5 mwaka huu, mpaka wakati huo kwa sehemu ambayo jengo limefika naamini litakuwa limekamilika,” alieleza Mwinjuma.

Amesema jengo hilo lipo katika hatua ya umaliziaji ambapo kwa sasa imebaki umaliziaji wa kuwekwa mifumo ya umeme, mifumo ya hewa, kuweka marumaru chini na madirisha, ambayo kati ya madirisha 120 yanayotakiwa kwenye jengo hilo, yameshawekwa madirisha takribani 75 huku mengine yakiwa katika hatua za umaliziaji.

Mwinjuma amesema ukaguzi alioufanya katika mradi huo ni maandalizi ya ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kukagua shughuli za TSN. “Tumeona maendeleo na mipango mbalimbali, maendeleo ya jengo letu na mitambo ambayo inakuja kufanya shughuli hii ya uchapaji na mipango mbalimbali ambayo TSN wanayo ili kwenda na kasi ya dunia inavyokwenda.

Tumejadiliana mambo kadhaa na wakandarasi na Menejimenti ya TSN na tumefikia muafaka, tupo tayari kwa kuipokea Kamati ya Bunge,” alisema Naibu Waziri. SOMA: Mambo yameiva mradi kiwanda cha uchapaji TSN

Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Asha Dachi alisema hadi sasa ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 71.2, na sehemu ya pili ya mradi huo ambayo ni mitambo ya kiwandani ambayo imekwisha wasili ikiwa imefikia asilimia 85.6. Amesema kiwanda hicho kinakwenda kuongeza ufanisi wa TSN kwa kuhakikisha TSN inachapa magazeti yake mwenyewe na kufanya biashara mbalimbali za uchapaji na kutoa huduma za uchapaji kwa wadau binafsi na serikali.

“Kamati ya Bunge inatarajiwa kuja kati ya tarehe 14 au 15, lakini TSN tupo tayari muda wowote ule kwa sababu ni mradi ambao unasukumwa kwa kasi kwa ufanisi mkubwa, kwa hiyo katika suala la ukaguzi tuko tayari muda wowote watakapokuja tutawapitisha waone ili waweze kupaza sauti zaidi ili mradi ukamilike,” alifafanua Dachi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button