Mambo yameiva mradi kiwanda cha uchapaji TSN

DAR ES SALAAM: MRADI wa ujenzi wa jengo la kiwanda cha uchapaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), umefikia asilimia 71., huku mitambo ambayo imeshawasili imefikia asilimia 85.6.

Taarifa hiyo imetolewa leo Machi 5, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Asha Dachi, mbele ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma katika ziara aliyoifanya ya kukagua mwendelezo wa ujenzi wa mradi huo.

Amesema mradi huo ni chanzo kingine cha mapato na unatarajia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa kampuni hiyo kwa kuhakikisha TSN inachapisha magazeti yake na kufanya biashara mbalimbali za uchapaji kwa taasisi, wadau binafsi na wa serikali.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Mwinjuma amesema ziara hiyo ililenga kutathmini maendeleo ya mradi pamoja na mipango inayotekelezwa, ambapo amesema endapo kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa, jengo hilo linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu.

“Ziara hii pia inalenga kuwaandaa kabla ya Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuja kukagua shughuli mbalimbali za TSN.

“Kama Naibu Waziri mwenye dhamana ya kusimamia taasisi hii, nimeona ni muhimu kupata ufahamu wa kina kuhusu maendeleo ya mradi huu,” amesema Naibu Waziri.




