‘Drone’ kutumika kudhibiti tembo Bariadi Vijijini

SIMIYU: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kuwa serikali itapeleka ndege nyuki (Drone) kwa ajili ya kufukuza Tembo ambao wamekuwa changamoto kwa wananchi wa jimbo la Bariadi Vijijini.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi, Kenan Kihongosi ameyasema hayo wakati akizungumzia changamoto hiyo iliyotolewa na Mbunge wa Bariadi Vijijini, Masanja Kadogosa.

Kihongosi amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo, serikali itapeleka ndege nyuki katika eneo hilo kwa ajili ya kufukuzia tembo.

Baada ya maelezo ya Kihongosi, Mbunge huyo aliishukuru serikali kwa hatua inazochukua kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ya kukabiliana na changamoto hiyo yenye lengo la kuwanusuru wananchi na tembo.

“Serikali imebuni njia mbalimbali kudhibiti tembo, hivi karibuni imesema itatumia ndege nyuki kuwarudisha, kama mnavyojua tembo huwa wanakuwa katika makundi wanapotembea hivyo kiongozi wao huwa anafungwa kitu fulani shingoni ambapo wanaweza kujua alipo, tutahakikisha tunatoa ushirikiano kutimiza hili,” amesema kadogosa.

Kihongosi amekagua mradi wa shamba la mfano la Mkulima, Charles Masunga lenye ekari 5 lililopo Mtaa wa Sanungu kata ya Somanda, akibainisha matumizi ya ndege nyuki katika kilimo yana tija kubwa.

“Ilani ya chama ilisema itaboresha sekta ya kilimo kupitia teknolojia bora ya kisasa ili kuongeza uzalishaji, pembejeo hivyo hatua hii ji muhimu sana kwa wakulima,”amesema.

Awali, Mkulima huyo aliwasilisha changamoto zinazomkabili ikiwemo barabara kutopitika na kushindwa kuvuna majira ya usiku kutokana na kuwepo changamoto ya umeme.

Akijibu changamoto hizo, Kenani alimwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo kuwasiliana na Tarura ili kutatua changamoto hiyo na kuwezesha barabara kupitika kwa urahisi pindi anaposafirisha pamba kwenda kwenye ghala.

Kuhusu changamoto ya kutokuwepo umeme, Kihongosi alimwagiza Meneja wa Tanesco kuhakikisha ndani ya siku saba umeme unawaka kwa nchi mkulima huyo ili kuwezesha shughuli za uvunaji pamba.

Naye, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Sylvanus Gwiboha alisema shamba hilo lina ekari 5 na kwamba matarajio nj kuvuna kilo 6,700,000 au tani 6,700 ikiwa ni ongezeko la kilo 1,650,640 kulinganisha na msimu uliopita ambao ilikuwa kilo 5,049,360 (2024/25).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button