JKCI, Selian wajipanga AFCON 2027

FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitafanyika mwaka 2027 kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Kutokana na hali hiyo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Selian (ALMC) ya jijini Arusha, zimeunda kamati maalumu ya kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za afya.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mashabiki wa mpira wa miguu pamoja na wananchi wanapata huduma bora za afya wakati wa mashindano hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha,  Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge, amesema hospitali hiyo inaendelea kufanya ukarabati wa vyumba vya Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), kuongeza vitanda vya kisasa pamoja na kusimika mitambo ya kisasa ya uchunguzi.

Amesema pia hospitali hiyo itatumia teknolojia ya Akili Unde (AI) ili kurahisisha mawasiliano kati ya madaktari na wagonjwa.

Wakati huo huo, Hospitali ya Selian (ALMC) kwa kushirikiana na JKCI zimeendesha kambi maalumu ya matibabu ya bure kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa ya figo, mfumo wa mkojo na mishipa ya damu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Figo Duniani

Akizungumza mjini hapa Dk Saleh Mwinchete, ambaye ni msimamizi wa JKCI Arusha,  amesema kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Machi 12 mwaka huu, huku huduma za matibabu bure zikitolewa kuanzia Machi 9 hadi 13, ambapo  madaktari bingwa zaidi ya 10 kutoka Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa kushirikiana na madaktari wa JKCI na ALMC wanashiriki kutoa huduma hizo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button