Serikali kupitia mapenddekezo 284 ya kodi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itayafanyia uchambuzi wa kina mapendekezo 284 ya maboresho ya mifumo ya kodi nchini kabla ya kuanza utekelezaji wake.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kupokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Mapendekezo ya Maboresho ya Kodi kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue, Rais Samia amesema mapendekezo hayo yanahitaji uchambuzi wa kina kabla ya utekelezaji wake. SOMA: Tume Maboresho ya Kodi yasheheni wabobezi kutimiza malengo
Amesema baadhi ya mapendekezo hayo yanahusisha marekebisho ya sheria mbalimbali, maboresho ya taasisi pamoja na uwekezaji wa awali katika utekelezaji wa mifumo mipya ya ukusanyaji wa kodi “Mapendekezo haya yanatupeleka kwenye sera na sheria za kodi ambazo zitalinda uchumi wetu na kuhakikisha ukusanyaji wa kodi hauhitaji gharama kubwa, bali unakuwa na ufanisi zaidi,” alisema Rais Samia.

Aliongeza kuwa Serikali inapanga kuyatekeleza mapendekezo hayo katika vipindi vitatu vya muda ambavyo ni muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kulingana na uzito na mahitaji ya kila pendekezo. “Nahitaji uchambuzi wa kina na tutajipanga kuyatekeleza kwa awamu tatu; muda mfupi kwa yale yasiyohitaji maandalizi makubwa, muda wa kati na muda mrefu kwa yale yanayohitaji mabadiliko makubwa,” alisema.

Aidha, Rais Samia amesema anatamani kuona maboresho hayo yanakamilika na kuacha misingi imara ya sera na mifumo ya kodi itakayoiwezesha nchi kufikia malengo yake ya maendeleo.
Tume ya Maboresho ya Kodi iliundwa mwaka 2024 na Rais Samia kwa lengo la kuchambua mfumo wa kodi uliopo na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kupunguza malalamiko kwa walipa kodi pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.



