Mbunge Kyela akabidhi gari huduma za jamii

MBEYA: Mbunge wa Jimbo la Kyela, Baraka Mwamengo, amenunua gari lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 50 na kulikabidhi kwa wananchi wa jimbo hilo kwa ajili ya huduma za kijamii, ikiwemo kusaidia wagonjwa na shughuli za misiba.
–
Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, Mwamengo amesema uamuzi wa kununua chombo hicho umetokana na changamoto mbalimbali ambazo wananchi wamekuwa wakikumbana nazo, hususan katika upatikanaji wa usafiri wa haraka wakati wa dharura.

Ameeleza kuwa mara nyingi wananchi wa Kyela wamekuwa wakipata ugumu wa kuwafikisha wagonjwa hospitalini kwa wakati au kushiriki ipasavyo katika shughuli za kijamii kutokana na ukosefu wa usafiri wa uhakika.
“Gari hili ni mali ya wananchi wote wa Kyela, litatumika kuwahudumia katika nyakati za shida bila ubaguzi,” amesema Mwamengo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephen Manase, amewataka wananchi kuhakikisha wanalitunza gari hilo ili liweze kudumu na kuwanufaisha kwa muda mrefu.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kumuombea mbunge huyo ili aweze kupata uwezo wa kuongeza huduma zaidi, ikiwemo kununua gari jingine la kusaidia jamii.
Wananchi wa eneo hilo wamepokea kwa furaha msaada huo, wakieleza kuwa utasaidia kupunguza adha ya usafiri hasa kwa maeneo ya vijijini ambayo hayana huduma za usafiri wa uhakika.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za viongozi hao kuboresha ustawi wa jamii na kusogeza huduma muhimu karibu zaidi na wananchi wake.



