Ujenzi kongani ya viwanda 150 kuanza Bagamoyo

DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetangaza kuanza rasmi kwa ujenzi wa kongani ya kisasa ya viwanda zaidi ya 150  Bagamoyo Eco Maritime City (BEMC), Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Akizungumza leo Aprili 9 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, alisema mradi huo unaotekelezwa na HWTZ SEZ Limited, tanzu ya Hongwang Holding Group ya China, unahusisha eneo la hekari 500 kwa mkataba wa upangishaji wa ardhi wa miaka 33.

Mradi utahusisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, umeme, mifumo ya maji taka, ulinzi na nishati mbadala ya jua, huku ukilenga kuvutia viwanda zaidi ya 150, ikiwemo uzalishaji wa magari, boti, pikipiki na vifaa vya ujenzi.

Utekelezaji wake unatarajiwa kuingiza uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 3, kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 5,000 kwa Watanzania, kuleta teknolojia za kisasa na kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa masoko ya ndani na nje ya nchi. Pia, mradi utatoa mafunzo kwa vijana katika vyuo maalum vya ufundi.

Teri amesema ujio wa wawekezaji wakubwa unaonyesha kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji Tanzania, ukichangia utulivu wa kisiasa, sera na sheria rafiki za biashara, na jitihada za serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya kuhamasisha uwekezaji Agosti 2025, TISEZA imepokea maombi 48, ambapo mikataba tisa tayari imesainiwa na wawekezaji walioanza hatua za utekelezaji.

Mamlaka inawahimiza wadau na vyombo vya habari kuendelea kuitangaza Tanzania kama kitovu cha uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button