Umeme waendelea kuimarika nchini

DAR ES SALAAM: JUHUDI za Serikali za kuongeza upatikanaji wa umeme nchini zimezaa matokeo makubwa, ambapo kiwango cha wananchi wanaopata huduma hiyo kimeongezeka kutoka asilimia 14 mwaka 2011 hadi asilimia 85 mwaka 2020.

Akizungumza katika Kongamano la Siku ya Nishati lililofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba), jijini Dar es Salaam, Mhandisi kutoka Wizara ya Nishati, Christopher Nyondo, amesema juhudi za kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha na kila mwananchi anafikiwa na huduma hiyo zilianza mara baada ya uhuru.

Amesema mwaka 1967 uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini ulikuwa megawati 21 pekee, hali iliyosababisha wananchi wachache kupata huduma ya umeme. Kufikia mwaka 2011, ni asilimia 14 tu ya Watanzania waliokuwa wameunganishiwa umeme, jambo lililoifanya Serikali kuongeza juhudi na uwekezaji katika sekta hiyo ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hiyo.

Nyondo amesema matokeo ya juhudi hizo yalionekana kufikia mwaka 2020, ambapo vijiji vyote nchini vilikuwa vimefikiwa na umeme, huku asilimia 85 ya Watanzania wakinufaika na huduma hiyo. Aidha, alisema mtandao wa usafirishaji wa umeme umeendelea kupanuliwa ili kuimarisha upatikanaji wa nishati katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Kongamano hilo limewakutanisha viongozi, watunga sera, wataalamu, wawekezaji, washirika wa maendeleo na wadau wa sekta ya nishati kujadili mwelekeo wa sekta hiyo, fursa za uwekezaji, ubunifu na teknolojia, pamoja na mchango wa sekta ya nishati katika kukuza uchumi wa taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button