Uchumi Afrika watajwa kushuka

BENKI ya Dunia imeeleza kuwa ukuaji wa uchumi katika mataifa ya Afrika yaliyopo Kusini mwa Jangwa la Sahara unatarajiwa kupungua kutoka asilimia 4.4 hadi 4.1 mwaka 2026, kutokana na athari za vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa wiki hii, hali hiyo itasababisha changamoto katika uagizaji wa bidhaa muhimu ikiwemo mafuta na mbolea, hali inayoweza kuongeza gharama za maisha na uzalishaji katika nchi nyingi za ukanda huo.
Ripoti imebainisha kuwa nchi zenye changamoto za kiuchumi na kifedha ndizo zitakazoathirika zaidi, zikiwemo Burundi, Malawi, Ethiopia, Kenya na Msumbiji. SOMA: Kida: Tafiti zisaidie kuimarisha uchumi
Aidha, imeelezwa kuwa kuna ongezeko la wasiwasi kuhusu hatima ya uwekezaji kutoka mataifa ya Ghuba katika bara la Afrika, hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki ambako yamekuwa yakifanya uwekezaji mkubwa katika sekta za madini, nishati mbadala pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
Ripoti hiyo inaonya kuwa hali ya sintofahamu ya kisiasa na kiusalama katika baadhi ya maeneo duniani inaweza kuendelea kuathiri mtiririko wa uwekezaji na biashara, hivyo kudhoofisha kasi ya ukuaji wa uchumi katika ukanda huo.



