Serikali Yatenga Bil.4.2 Tuzo ya Uandishi

SERIKALI imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, ambapo jumla ya shilingi bilioni 4.2 zimetengwa katika kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Carolyne Nombo amesema fedha hizo zimetumika kugharamia uendeshaji wa tuzo, uchapishaji wa vitabu vilivyoshinda pamoja na utoaji wa zawadi kwa washindi. “Hakika tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia Wizara fedha kwa ajili ya uendeshaji wa tuzo hii,” alisema Profesa Nombo. SOMA: Tuzo ya Nyerere mshindi kunyakua mil10
Hatahivyo amesema Wizara inapanga kushirikiana na vyuo vikuu pamoja na idara za fasihi kuendesha warsha kwa waandishi chipukizi na kuandaa kongamano la kitaifa la uandishi bunifu, hatua itakayosaidia kuongeza hamasa ya uandishi na kukuza sekta ya uchapishaji nchini.
Amesisitiza kuwa uwekezaji huo umechangia kuongeza ari ya waandishi na kuimarisha sekta ya uandishi na uchapishaji, ambayo ni miongoni mwa malengo makuu ya tuzo hiyo. Pia ametoa wito kwa Watanzania kuendeleza utamaduni wa kusoma na kuandika vitabu ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza maarifa na ubunifu nchini.



