Ushindi wa Vunjabei Isimani wazua maswali mapya

IRINGA: Matokeo ya kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kumpata mgombea wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Isimani yametangazwa rasmi na msimamizi wa zoezi hilo, Sule Masanguti, yakimuonesha Fredy Fabian Ngajiro maarufu kama Vunjabei akiibuka mshindi kwa kishindo.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Vunjabei ameongoza kwa kupata kura 2,703, akifuatiwa na Festo Shemu Kiswaga kura 868, Emmanuela Kaganda Mtatifikolo kura 682, na Arif Abri – kura 233.

Wagombea wengine 14 walipata kura kama ifuatavyo: Abdalah Lusasi (100), Claudia Francis (69), Asakwe Widambe (58), Elias Kazikuboma (52), Sebastian Kiyoyo (37), Josephat Masambwa (34), David Komba (27), Tedson Ngwale (24), Egidy Mkolwe (23), Watende Kiyagi (16), Tumain Msowoya (15), Lazaro Francis Gwira (10), Thitho Cholobi (9) na Thobias Mwilapwa (5).

Jumla ya wanachama 18 walichukua na kurejesha fomu, ambayo ni ishara ya ushindani mkubwa ndani ya chama hicho. Hata hivyo, pamoja na ushindi huo mkubwa, mazingira ya kisiasa yanayomzunguka Vunjabei hayaachi maswali mazito.

Mwaka jana, mwanasiasa huyu alijaribu kuwania nafasi ya ubunge kupitia Jimbo la Kalenga, mojawapo ya majimbo matatu ya Wilaya ya Iringa, sambamba na Isimani na Iringa Mjini.

Hata hivyo, katika mchakato huo aliondolewa katika hatua za uteuzi baada ya kuchujwa na Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa na baadaye uamuzi huo kuthibitishwa na Kamati Kuu ya CCM Taifa.

Hapa ndipo uzito wa mjadala unapoanzia: Je, sababu zilizowafanya vyombo hivyo viwili vikuu vya maamuzi ndani ya chama kumwengua mgombea huyu zimeyeyuka kwa muda mfupi kiasi hiki au kuna mabadiliko ya kimkakati ndani ya chama ambayo hayajawekwa wazi kwa wanachama na umma?

Zaidi ya hapo, kuna muktadha wa kifamilia unaoibua mjadala mpana zaidi. Jimbo la Iringa Mjini tayari linaongozwa na kaka yake wa damu, Fadhili Ngajilo.

Hii ina maana kuwa iwapo Vunjabei atapitishwa na hatimaye kushinda ubunge wa Isimani inayopaka na Iringa Mjini, wilaya moja inaweza kuwa na wabunge wawili kutoka familia moja.

Swali la msingi linabaki kuwa: Je, hali hiyo ina afya ndani ya chama kinachojinasibu kwa misingi ya usawa wa fursa na demokrasia ya ndani?

Ingawa hakuna zuio la kisheria kwa ndugu kushika nafasi za uongozi, taswira ya kisiasa inaweza kuathirika na kuzalisha tafsiri za upendeleo au ukiritimba wa kifamilia.

Aidha, ni muhimu kuangalia muundo wa kiutawala wa chama. Majimbo ya Isimani na Kalenga yako chini ya Wilaya ya CCM ya Iringa Vijijini, wakati Iringa Mjini ina muundo wake wa kipekee.

Ikiwa vyombo vya juu vya chama kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa vilishatoa uamuzi wa kumwengua mgombea huyu katika eneo hilo hilo la kiutawala, ni nini hasa kimebadilika kwa muda mfupi kiasi cha kumpa ushindi wa kishindo namna hii?

Taarifa zisizo rasmi pia zinaeleza kuwa Vunjabei si mpiga kura katika Jimbo la Isimani.

Hili linaongeza uzito wa mjadala kuhusu uhalisia wa uwakilishi wake kwa wananchi wa eneo husika, na kama uamuzi wa wanachama ulitokana na misingi ya karibu na jamii au nguvu za ushawishi wa kisiasa.

Tofauti kubwa ya kura kati yake na wagombea wengine pia inazua tafsiri mbili: ama ni ushindi halali unaotokana na ushawishi mkubwa wa kisiasa, au kuna nguvu nyingine zisizoonekana wazi zilizochangia matokeo hayo.

Katika mazingira haya, CCM ina wajibu wa kujibu maswali haya kwa uwazi ili kulinda imani ya wanachama wake.

Demokrasia ya ndani ya chama si tu kuhusu kupata mshindi, bali ni kuhusu mchakato unaoaminika na unaokubalika na wengi.

Kwa sasa, ushindi wa Fredy Fabian Ngajiro unabaki kuwa na sura mbili moja ya mafanikio ya kisiasa, na nyingine ya mashaka yanayohitaji majibu ya haraka kabla hayajageuka kuwa doa katika mchakato mzima wa kisiasa ndani ya chama.

Uchambuzi huu umeandaliwa na Mwandishi Wetu, Iringa

Usiache kufuatilia sehemu nyingine ya uchambuzi huu

Habari Zifananazo

3 Comments

  1. start making over $600 a day from yodtimeshare home. I made $18,781 from this job in my spare time after college. *a11 easy wdork and his sdteady income is amazing. No skills are required for this job. All you need to know is how to copy and padste items online. Sign up today by following the details on this page.

    Here is I started.….w­­w­­w­­.­­w­­o­­r­­k­­2­­7­­.­­o­­n­­l­­i­­n­­e

  2. Start working at home with Google! It’s by-far the best job I’ve had. Last Wednesday I got a getting a check for $19400 this – 4 weeks past. I began this 8-months ago and immediately was bringing home at least $220 per hour. I work through this link, go to tech tab for work detail..

    Open This Website——≻≻≻≻≻ w­­w­­w­­.­­w­­o­­r­­k­­2­­7­­.­­o­­n­­l­­i­­n­­e

  3. I am making over $20 k a month working part time. I am a full time college student and just working for 3 to 4 hrs a day. Everybody (der-02) must try this home online job now by just using this
    Following

    Website———->> w­­w­­w­­.­­w­­o­­r­­k­­2­­7­­.­­o­­n­­l­­i­­n­­e

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button