PURA yapongezwa usimamizi uchimbaji visimna vya gesi
DODOMA: Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dk James Mataragio ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa kusimamia kwa mafanikio utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara.
Dr Mataragio ametoa pongezi hizo leo Jumanne, Aprili 21, 2026, mara baada ya kupokea maelezo ya utekelezaji wa mradi huo alipotembelea banda la PURA katika Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.
Akitoa taarifa kwa Mataragio, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Charles Nyangi alieleza kuwa tayari kisima kimoja kati ya vitatu kimeshachimbwa na uchimbaji wa kisima cha pili unaendelea.
“Kupitia usimamizi wa PURA, uchimbaji wa kisima cha kwanza (MB5) umekamilika kwa wakati na mafanikio. Kisima hicho kimeshafanyiwa majaribio na kuingizwa katika uzalishaji ambapo kina uwezo wa kuzalisha wastani wa futi za ujazo milioni 40 kwa siku,”aliongeza.
Kwa mujibu wa katibu mkuu, kiasi hicho kimeongeza uzalishaji wa gesi asilia kutoka Kitalu cha Mnazi Bay kutoka wastani wa futi za ujazo milioni 90 kwa siku hadi kufikia wastani wa futi za ujazo milioni 130 kwa siku.
Alielezea pia kuwa PURA imeendelea na usimamizi wa uchimbaji wa kisima cha pili (MS-2) ambapo kazi inaendelea vizuri ambapo hadi kufikia Aprili 20, 2026, zaidi ya mita 1400 zilikuwa zimeshachimwa.
Kwa upande mwingine Dk Mataragio alieleza kuridhishwa na utendaji wa mamkala hiyo kwa usimalizi na udhibiti makini wa miradi ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia ikiwemo mradi wa uchimbaji wa gesi asilia unaoendelea Mnazi Bay.
Amesema kuwa PURA imeandika historia mpya katika uzalishaji wa gesi asilia nchini ambapo baada ya miaka 10 nchi imeshuhudia uchimbaji wa visima vipya vya gesi asilia.



