Matumizi akili mnemba yaongeza ufanisi UDSM

DAR ES SALAAM:  Matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba yameelezwa kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha ufanisi wa taasisi, huku Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kikichukua hatua za makusudi kuboresha huduma na utendaji kupitia mifumo ya kidijitali.

Akizungumza Aprili 22, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano Maalumu wa Baraza la Wafanyakazi wa UDSM, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Moremi Marwa, amesema katika zama za mabadiliko ya haraka, teknolojia ina nafasi kubwa katika kurahisisha kazi na kuongeza tija.

Ameeleza kuwa matumizi ya Akili Mnemba yana mchango mkubwa katika kuboresha ubora wa huduma pamoja na kuimarisha maamuzi ya kitaasisi. Aidha, amewahimiza wafanyakazi wa chuo hicho kujifunza na kutumia teknolojia hizo katika majukumu yao ya kila siku ili kuongeza ufanisi.

“Teknolojia, hususan hii ya akili mnemba, ina nafasi kubwa katika kurahisisha kazi, kuongeza ubora wa huduma na kuboresha maamuzi ya kitaasisi. Hivyo nawapongeza na kuwahimiza wafanyakazi wote kujifunza na kutumia teknolojia hizi,” amesema Marwa.

Mbali na hilo, Marwa amesisitiza umuhimu wa uadilifu na uwajibikaji kwa watumishi, akieleza kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kujenga imani kwa jamii pamoja na wadau wa chuo.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, amesema chuo kimepata mafanikio katika maeneo manne muhimu, yakiwemo kuimarika kwa mifumo ya ndani, udhibiti wa kifedha, utambuzi wa watumishi na ustawi wa wanajumuia wa chuo.

Amebainisha kuwa katika kuimarisha nidhamu ya fedha, chuo kimefanikiwa kupata hati safi za ukaguzi kwa miaka minne mfululizo, huku idadi ya hoja za ukaguzi ikipungua kutoka 86 hadi 34.

Aidha, Prof. Anangisye amesema chuo kinaendelea kunufaika na mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu kwa Uchumi (HEET), ambao umechangia kuboresha miundombinu ya kufundishia, kuimarisha utafiti na kuharakisha mageuzi ya kidijitali.m

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button