TFS yaanzisha utalii ikolojia hifadhi ya mikoko Tanga

TANGA: WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imetenga Sh milioni 578 kwa ajili ya kutekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu na huduma za utalii katika hifadhi ya mikoko jijini Tanga.

Mhifadhi wa Mwandamizi wa TFS Wilaya ya Tanga, Lawrence Brighton amesema hayo akielezea utekelezaji mradi huo wa kimkakati kwa lengo la kukuza sekta ya utalii wa ikolojoa na fukwe mkoani Tanga.

Brighton amesema hifadhi hiyo ya kipekee inapatikana katika eneo la Sahare ambako Bahari ya Hindi inakutana na misitu ya mikoko.

“Utekelezaji wa mradi huu unalenga kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya utalii Tanzania,” amesema Brighton.

Amesema mradi wa ujenzi wa miundombinu umehusisha ujenzi wa daraja la mbao ya mikoko lenye  urefu wa mita 350 lililojengwa juu ya maji ili kitoa fursa ya wageni kutembea juu ya maji na kuona mazingira ya ufukwe za Pwani ya Bahari ya Hindi.

Brighton ametaja Miundombinu nyingine muhimu ambayo imejengwa ili kuboresha huduma kwa watalii ni pamoja na mgahawa wa kisasa uliopo juu ya maji, vyoo vya kisasa pamoja na sehemu maalumu kwa ajili ya kupigia picha.

Amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo umetekelezwa kwa weledi mkubwa na  mazingira, kuepusha ukataji miti mkubwa ili kulinda mfumo wa ikolojia unaozunguka eneo hilo.

Brighton akieleza kwa kina zaidi juu ya utekelezaji huo alisema  umetekelezwa kwa awamu mbili kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii.

“Katika awamu ya kwanza iliyofanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2024/25 TFS ilifanikiwa kujenga   mita 150 za daraja kwa kutumia mapato yake ya ndani,” amesema Brighton.

Amesema Serikali, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, ilitoa fedha za ziada kwa ajili ya kukamilisha awamu ya pili ya ujenzi huo, ambapo kwa sasa daraja limejengwa kwa urefu wa mita 350.

Brighton amesema kukamilika kwa maboesho hayo kumeongeza idadi ya watalii wanaotoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa ajili ya kutembelea eneo hilo la kuvutia.

“Tangu kuwekwa kwa miundombinu hii ya ubunifu mkubwa wa kuvutia eneo limekuwa likowavutia watalii wengi, ambapo takwimu zetu zinaongesha zaidi ya wageni 19,500 kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na  nje ya mkoa  wametembelea kivutio hiki tangu mwezi Julai, 2025, hadi Machi 2026  ameeleza  Brighton.

Pia amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian kwa kisimama mstari wa mbele katika kulitangaza eneo hilo, hatua ambayo imeendelea kuwavutia wadau mbalimbali kutembelea kivutio hicho.

Kwa upande wake Ofisa Utalii wa TFS , Michael Charles, amezema huduma za kutalii kwa bodi ya mwendokasi, uvuvi wa samaki na kuogelea ni miongoni mwa shughuli zinazowavutia wageni wengi kutembelea eneo hilo.

“TFS imeamua kuwekeza katika eneo hili linalojulikana kwa jina maarufu la Mangrove Boardwalk ili kukuza utalii wa fukwe kaskazini mashariki mwa Tanzaniani, eneo hili ni tulivu linalofaa kwa matembezi ya asili, upigaji picha, na mapumziko,”  amesema Charles.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button