Kura za maoni Isimani zaendelea kuzua sintofahamu

IRINGA: Kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Isimani zimeibua mjadala mzito unaotikisa si tu uhalali wa matokeo, bali pia misingi ya demokrasia ya ndani ya chama hicho tawala.
Kilichopaswa kuwa zoezi la kidemokrasia la kuchuja wagombea bora, kimeelezwa na baadhi ya wanachama wa jimbo hilo kuwa tukio linaacha maswali mengi kuliko majibu.
Wajumbe kadhaa waliohusika katika kura hizo wamejitokeza wazi kuhoji mchakato mzima, wakidai kuwa walilazimika kupiga kura kwa majina ya watu ambao hawakuwaona, kuwasikia wala kuwauliza maswali.
Kauli za wajumbe kama Akiyalii Mrongaa na Dotto Kidole kutoka Ilolompya zinaakisi hali halisi ya sintofahamu iliyotawala.
Wanasema hawakupewa fursa ya msingi kabisa katika demokrasia kusikiliza sera na kupima uwezo wa wagombea hao na badala yake, walijikuta wakifanya maamuzi gizani, wakiongozwa na majina badala ya hoja.
“Je, kura hizi zilikuwa ni chaguo la wajumbe au utekelezaji wa matakwa yaliyopangwa nyuma ya pazia,” aliuliza Kidole.
Tuhuma za uwepo wa viashiria vya rushwa nazo zimeongeza doa katika mchakato huo.
Kauli ya Alphonce Mdindile kutoka Magozi kuhusu gari lililodaiwa kusambaza fedha kwa baadhi ya wajumbe inazua picha ya ushindani usio sawa.

Ikiwa madai haya yana ukweli wowote, basi matokeo yaliyopatikana hayawezi kutenganishwa na ushawishi wa kifedha.
Hata hivyo, uongozi wa chama kupitia Katibu wa Wilaya ya Iringa, Sure Mwasanguti, umetetea mchakato huo kwa kueleza kuwa wagombea wote 18 ni wenyeji na wanafahamika.
Alisema wanachoamini huo ni uchaguzi wa kuziba nafasi na kwamba wana Isimani wanawafahamu wagombea hao kwasababu sehemu yao walishiriki kura za maoni zilizopita.
Lakini hoja hiyo imepuuzwa na Mdindile akisema inapuuzia kiini cha malalamiko—kwamba kufahamika kwa jina hakutoshi kuwa mbadala wa mjadala wa wazi wa sera na uwezo.
Katika kura hizo za maoni, Vunjabei ameongoza kwa kupata kura 2,703, akifuatiwa na Festo Shemu Kiswaga kura 868, Emmanuela Kaganda Mtatifikolo kura 682, na Arif Abri kura 233.

Wagombea wengine 14 walipata kura kama ifuatavyo: Abdalah Lusasi (100), Claudia Francis (69), Asakwe Widambe (58), Elias Kazikuboma (52), Sebastian Kiyoyo (37), Josephat Masambwa (34), David Komba (27), Tedson Ngwale (24), Egidy Mkolwe (23), Watende Kiyagi (16), Tumain Msowoya (15), Lazaro Francis Gwira (10), Thitho Cholobi (9) na Thobias Mwilapwa (5).
Kwa mujibu wa Kidole matokeo yaliyompa ushindi mkubwa Fredy Fabian Ngajiro maarufu kama Vunjabei, dhidi ya wapinzani wake waliobaki mbali kwa tofauti kubwa, yamezua tafsiri mbili: ama alikuwa na mvuto wa kipekee usio na mpinzani, au kulikuwa na nguvu nyingine zilizocheza nyuma ya pazia.
Uchambuzi huu umeandaliwa na mwandishi wetu kutoka Iringa
Uchambuzi mwingine utakujia.



