Kampeni usalama barabarani yazinduliwa

DAR ES SALAAM:KATIKA jitihada za kupunguza ajali na kuimarisha usalama barabarani, Kampuni ya Azam TV imezindua rasmi kampeni ya usalama barabarani katika Wilaya ya Ubungo, ikilenga kuwahamasisha waendesha bodaboda kuzingatia sheria na kujilinda wanapokuwa barabarani.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Ofisa Usafirishaji Barabarani, Amina Kikala amesisitiza umuhimu wa waendesha bodaboda kujipenda na kulinda afya zao binafsi.

Amesema kuwa madereva hao wanapaswa kutambua kuwa kuna watu wanaowategemea, hivyo wanatakiwa kuepuka mwendo kasi unaoweza kuhatarisha maisha yao.

“Unapokuwa barabarani, tambua kuna familia inakutegemea. Usifanye haraka ambayo inaweza kukatisha maisha yako,” amesema Kikala.

Aidha, amewataka waendesha bodaboda kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga kama vile kofia ngumu (helmet), makoti ya usalama, pamoja na kuvaa viatu vinavyofaa wakati wa kazi.

Pia amesisitiza umuhimu wa kufuata sheria za barabarani na kuepuka kubeba mizigo au abiria kupita kiasi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Azam TV, Yahaya Mohamed, amesema kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii, kwa kutambua mchango wa watanzania wanaoendelea kuunga mkono huduma za kampuni hiyo.

“Tunafanya haya kama sehemu ya kurudisha shukrani kwa jamii inayotuzunguka,” amesema Yahaya.

Naye Mkurugenzi wa Mauzo wa Azam TV, Sabrina Mohamed Ally, amezindua rasmi kampeni hiyo ijulikanayo kama “Usalama Daima”, huku akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuongeza uelewa wa usalama kwa waendesha vyombo vya moto na kupunguza ajali zisizo za lazima.

Katika kampeni hiyo, Azam TV pia imegawa makoti ya usalama kwa waendesha bodaboda ili kuwasaidia kuongeza ulinzi wao wanapokuwa barabarani.

Mkuu wa Dawati la Masuala ya Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Dina Mosi amewataka madereva wa bodaboda kuzingatia tahadhari wanapokuwa barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima. Amesisitiza umuhimu wa kufuata sheria za barabarani, ikiwemo kutumia upande sahihi wa barabara wakati wa uendeshaji.

Mosi ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usalama barabarani iliyoandaliwa na Kampuni ya Azam Media Limited, inayolenga kutoa elimu kwa watumiaji wa vyombo vya moto, hususan madereva wa pikipiki.

Amesema elimu hiyo ni muhimu katika kupunguza ajali na kulinda maisha ya madereva pamoja na watumiaji wengine wa barabara, huku akihimiza ushirikiano kati ya wadau mbalimbali ili kuimarisha usalama barabarani nchini.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. [ JOIN US ] I get paid more than $90 to $300 per hour for working online. I heard about this job 3 months ago and after joining this I have earned easily $10k from this without having online working skills . Simply give it a shot on the accompanying site…
    .
    You can check more.======= http://www.giftpay7.vip

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button