Nyalandu: Tuimarishe mshikamano kulinda amani ya taifa

MSHAURI wa Rais wa Diplomasia, Balozi Lazaro Nyalandu amewaomba watanzania kudumisha na kulinda amani ya Taifa.

Balozi Nyalandu alisema hayo hivi karibuni wakati wa mahojiano malumu.

“Katika kipindi ambacho dunia inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama na utulivu wa mataifa mbalimbali, serikali imeendelea kusisitiza jukumu lake la msingi la kulinda maisha na mali za wananchi.” alisema.

Nyalandu, ameeleza kuwa msimamo wa serikali unaakisi dhamira ya dhati ya kuhakikisha kila mwananchi anaishi kwa amani na usalama, bila kujali changamoto zinazoweza kujitokeza.

Balozi Nyalandu amebainisha kuwa kauli ya Rais, Dk Samia Suluhu Hassan, inaonyesha wazi nia ya serikali kuendeleza utulivu wa nchi kwa kuweka mbele maslahi ya wananchi na kudumisha mshikamano wa kitaifa.

Aidha, aligusia umuhimu wa Ripoti ya Tume ya Jaji Chande, akieleza kuwa imekuwa chombo muhimu katika kuweka wazi ukweli uliokuwa ukizua maswali kwa muda mrefu miongoni mwa wananchi. Kupitia uchunguzi wa kina, tume hiyo imeainisha hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali katika kushughulikia changamoto zilizokuwepo, jambo linaloashiria uwajibikaji na uwazi.

Katika muktadha huo, Nyalandu amehimizwa wananchi kutambua tofauti kati ya haki ya kuandamana kwa amani na vitendo vya vurugu vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa. Ushirikiano kati ya jamii na vyombo vya dola umeelezwa kuwa nguzo muhimu katika kudumisha amani.

“Ni wajibu wa kila mmoja kuwa macho na kuepuka kushawishiwa kushiriki katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha ustawi wa taifa,” alisisitiza.

Kwa ujumla, Nyalandu amesema ulinzi wa taifa si jukumu la serikali pekee bali ni wajibu wa kila mwananchi. Kupitia mshikamano, inawezekana kujenga jamii yenye amani, umoja na maendeleo endelevu.

Amesema ni wakati wa kusimama pamoja, kuilinda nchi, na kuhakikisha mustakabali wa vizazi vijavyo unabaki kuwa salama na thabiti.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button