Vikwazo biashara vyatajwa kuathiri mauzo ya Tanzanite

DODOMA: Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema mwenendo wa biashara ya madini ya Tanzanite duniani umeendelea kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa masoko ya uhakika, hali inayochangiwa na vikwazo vya kibiashara pamoja na uwepo wa vito vinavyotengenezwa viwandani.
Amesema changamoto hiyo imesababisha kushuka kwa bei ya Tanzanite kutoka wastani wa Dola za Marekani 2,433.96 kwa kilogramu katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025 na kufikia Dola za Marekani 2,270.44 kwa kilogramu katika kipindi kama hicho mwaka 2025/2026, sawa na upungufu wa asilimia 6.72.
Waziri Mavunde ametoa maelezo hayo leo Jumatatu Aprili 27, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Aidha, waziri huyo amebainisha kuwa mahitaji ya madini mkakati na muhimu kama lithium, cobalt, nickel na rare earth elements yameendelea kuongezeka duniani kutokana na matumizi yake katika teknolojia za kisasa na nishati safi.
Alieleza kuwa hali hiyo inaipa Tanzania fursa ya kuongeza thamani ya madini hayo ndani ya nchi, hatua itakayosaidia kukuza mapato, ajira na mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.



