Ubunifu watakiwa ukusanyaji kodi

DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa katika jitihada za kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi, kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko ya kimfumo na kiusimamizi pamoja na kuibua mawazo ya kibunifu, hasa kutoka kwa vijana, ili kuendana na ukuaji wa biashara na teknolojia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya shindano la mawazo ya kibunifu kwa lengo la kukuza makusanyo ya kodi, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema kuwa tayari hatua za mabadiliko zimeanza kuchukuliwa kwa kushirikisha wabunifu na wafanyabiashara.

Amesema ushirikiano huo unalenga kuhakikisha mamlaka hiyo inaendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika uendeshaji wa biashara.

Kwa upande wake, Ephraim Mdee kutoka Idara ya Utafiti na Ubunifu ya TRA amesema kuwa katika awamu hiyo, washiriki ambao wengi wao ni vijana wanatarajiwa kuwasilisha mawazo yatakayosaidia kupanua wigo wa makusanyo ya kodi.

Ameeleza kuwa mawazo hayo yatapitia uchambuzi wa kamati maalum kabla ya kupatikana mshindi, ikiwa ni njia ya kuendelea kupata mbinu mpya za kuendesha mamlaka hiyo kwa ufanisi zaidi.

Baadhi ya vijana wabunifu walioshiriki katika mpango huo wamesema wako tayari kushirikiana na serikali kubuni na kuendeleza mawazo yatakayosaidia taifa, hususan katika kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button