Wazee wajitosa kushiriki mashindano ‘West Kill Forest’

KILIMANJARO: WANAMICHEZO na wapenzi wa utalii ikolojia zaidi ya 350 wakiwemo wazee wenye umri mkubwa wamejitokeza kujisajili ili kushiriki mashindano West Kili Forest Tour Challenge 2026,.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shamba la Miti Magharibi mwa Kilimanjaro chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yamatarajiwa kufanyika Juni 20 na 21 mwaka huu (2026) katika maeneo ya chini ya mlima Kilimanjaro, wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro.
Ofisa Utalii na Mratibu wa mashindano hayo kutoka Msitu wa Hifadhi Magharibi mwa Kilimanjaro, Mensieur Elly, amesema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na usajili bado uko wazi kwa washiriki wa ndani na nje ya nchi.
Elly amesema kwa mwaka huu mashindano hayo yatapambwa na wazee 57 waliochanguliwa na kuijiandikisha ambao wataongoza matembezi ya kilometa tano wakiwemo wenye umri zaidi ya miaka 93.

“Wazee hawa kwanza wataeleza historia ya eneo hili na kisha kuongoza matembezi ya kilometa tano na mwenye umri wa chini ni miaka 73 na wengine wamekuwa na miaka 93,” amesema Elly.
Amesema tukio hilo la kila mwaka,linalenga kuhamasisha uhifadhi wa misitu, maendeleo ya michezo na ukuaji wa uchumi wa kijani.
Elly amesema mashindano hayo ya siku mbili, yanayotarajiwa kuhudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Siha.
Amesema mashindano hayo yatahusisha utalii wa michezo mbalimbali ikiwemo matembezi ya milimani (hiking), mbio za kuanzia kilomita 5, 12 na 28 kwa mbio za baiskeli na pikipiki.
“Hadi mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu wanariadha zaidi 350 wamethibitisha kushiriki wakiwemo kutoka nje ya nchi ikiwemo Uhispania,”amesema Elly .
Elly amesema kuwa mashindano hayo yanaunganisha michezo na utalii wa matukio, yakilenga kuonesha bioanuai tajiri na uzuri wa asili wa mfumo wa ikolojia wa Magharibi mwa Kilimanjaro.
“Mbali na michezo, kutakuwa pia na ngoma za asili, vyakula vya kienyeji na maonesho ya sanaa za utamaduni ili kukuza urithi wa eneo hili,” amesema Elly.
Amesema tukio la mwaka jana lilivutia zaidi ya washiriki 557, wakiwemo wageni kutoka Kenya na Uganda pamoja na watalii wa kimataifa kutoka Ujerumani na Scotland.
Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti West Kilimanjaro, Robert Faida, amesema lengo la mashindano hayo ni kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa kulinda mfumo wa ikolojia wa Kilimanjaro huku yakihamasisha utalii endelevu katika eneo hilo.
Amesema mpango huo unalenga kuimarisha ushiriki wa jamii katika uhifadhi wa mazingira kupitia michezo na shughuli za utalii wa mazingira.
Faida pia amesema mashindano hayo yanaenda na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kukuza uchumi wa kijani ikiwa na kuhakikisha misitu inanufaisha kizazi cha sasa na kijacho.



