Wataalamu wajengewa uwezo matumizi mashine za mkaa mbadala

MOROGORO: JESHI la Magereza nchini limewapatia wataalamu wake ambao ni askari mafunzo maalumu ya matumizi ya mashine za kutengeneza mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya mimea kufuatiwa kununuliwa mashine za kisasa 61 zilizogharimu zaidi ya Sh milioni 900 na kusambazwa katika magereza 129 yaliyopo nchini.
Kamishna wa Fedha na Mipango wa Jeshi hilo ( CP), Chacha Bina, amesema hayo kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, Jeremiah Katungu wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya mashine za kutengeneza mkaa mbadala.

Mafunzo hayo ya siku nne yametolewa na wataalamu kutoka Kampuni ya Kuja na Kushoka TOOLS Manufactures Limited na Hanny G Investment kwa wataalam wa Jeshi hilo amba o ni askari na kufanyika katika Ukumbi wa Bwalo la Gereza Kihonda, mkoani Morogoro
Amesema mafunzo hayo ni ya kimwelekeo wa Kisera, Kiuchumi, Kimazingira, Kiusalama na yanaakisi dhamira ya Serikali ya awamu ya Sita chini Rais Dk Samia Suluhu Hassan na Amiri Jeshi Mkuu.

Lengo ni kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kinara katika matumizi ya nishati na teknolojia na ubunifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Amesema Serikali imeweka msisitizo mkubwa katika matumizi endelevu ya rasilimali , ulinzi wa mzingira na mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia umepewa kipaumbele cha juu kwa kutambua athari za kiafya, kiuchumi na kimazingira zitokanazo matumizi ya nishati zisizo safi.

Kamishna Chacha amesema Serikali imechukua hatua madhubuti kuhakikisha mabadiliko yanafanyika kwa kasi kwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa wa kupikia kwani Taasisi za Umma nchini, ikiwemo Jeshi la Magereza ambalo limeitikia wito huo kwa vitendo.
“Hadi sasa Magereza yote 129 nchini yanatumia nishati Safi ya kupikia ikiwemo Mkaa mbadala, Gesi vunde (Biogas), Gesi ya LPG, Gesi asilia na kuachana na matumizi ya kuni,”amesema Kamishna Chacha.

Amesema hatua hiyo itaongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wake katika kuzalisha nishati mbadala kwa kutumia rasilimali zilizopo za mabaki ya mimea ,kwani ni mzalishaji mkubwa wa mabaki ya mimea kupitia shughuli za kilimo na viwanda zinazofanyika katika Magereza mbalimbali nchini .
“Mabaki haya ambayo kwa miaka mingi hayakuwa yakitumika ipasavyo , sasa yatapata thamani mpya kupitia teknolojia hii ya kisasa ya kutengeneza mkaa mbadala,”amesema Kamishna Chacha.
Mbali na hayo ametoa shukrani kwa ushirikiano unaotolewa na wadau mbalimbali wa Maendeleo ikiweko Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Kampuni ya Kuja na Kushoka Ttools Manufacturers Limited, ambao waliwezesha ununuzi, utengenezaji na usambazaji wa mashine 61 zilizogharimu Sh milioni 914 za kuzalisha mkaa mbadala.
Kwa upande wake Kamishna wa Huduma za Urebu katika Jeshi hilo, Kamishna Amina Kavirondo amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wataalam wa Jeshi hilo kwani yanatoa fursa ya kuwajengea ujuzi wafungwa.
Amesema kuwa wafungwa watapata stadi za maisha zitakazowezesha kujiajiri na kushiriki katika shughuli halali za kiuchumi baada ya kumaliza vifungo vyao.
Kamishna Kavirondo amesema kuwa mkaa mbadala unaweza kuwa bidhaa ya kibiashara na chanzo muhimu cha pato kwa jeshi na taifa kwa ujumla.



