Kafulila azungumzia sekta ya afya

DAR ES SALAAM: Katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani, Mkurugenzi wa wa Kituo Cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPC) David Kafulila amesema kuwa ubora wa rasilimali watu, hasa afya na maarifa, ndio sarafu kuu ya dunia ya sasa na ndiyo njia pekee ya Tanzania kujiunga na nchi zenye uchumi wa zaidi ya Dola trilioni 1 ifikapo 2050.

Amesema wauguzi ndio nguzo ya rasilimali watu na mhimili muhimu wa uchumi huo, kwa kuwa bila afya bora hakuna tija kazini.

“Uuguzi si kazi tu, bali ni wito wa kitume unaohitaji upendo, subira na utu wa hali ya juu. Wauguzi ni daraja kati ya wagonjwa na kupona, wakiwa mstari wa mbele kuokoa maisha,” imeelezwa katika ujumbe wa maadhimisho hayo.

Tanzania inalenga kujiunga na “Club” ya nchi zenye uchumi wa kuanzia dola trilioni 1 ifikapo 2050. Ili kufikia lengo hilo, wataalamu wanasema nchi inahitaji kuongeza kwa kasi uwekezaji katika wauguzi ili kufikia kiwango cha Shirika la Afya Duniani cha wauguzi 45 kwa kila watu 10,000.

Kwa sasa wastani wa Afrika ni wauguzi 18 kwa kila watu 10,000, huku nchi tajiri zikiwa zimefika 100 kwa kila watu 10,000.

Pamoja na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu, vifaa tiba, dawa na ajira za wataalamu wa afya, bado changamoto ya uwiano wauguzi kwa idadi ya watu ipo kubwa. Wadau wanasema Serikali peke yake haiwezi kutatua pengo hilo.

Sekta binafsi yaitwa mezani

Takwimu zinaonesha sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70, sawa na Sh trilioni 334, ya gharama za Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2026/27-2030/31. Zaidi ya asilimia 50 ya matumizi ya afya nchini yanatoka sekta binafsi, na karibu asilimia 40 ya vituo vya afya vinamilikiwa au kuendeshwa na sekta hiyo.

“Katika juhudi za kuongeza uwezo wa kugharimia sekta muhimu kama afya na elimu kwa masikini, tunaendelea kusisitiza PPP ili Serikali iendelee kuachana na kuwekeza maeneo yenye mvuto wa sekta binafsi na anachokiokoa kisaidie maeneo kama afya kwa masikini ambayo hayana mvuto kibiashara lakini ni muhimu kwa uchumi na ustawi wa Taifa,” walisema wadau.

Amesema kuwa dhana ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi inasisitizwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku wakiwataka wananchi pia kushiriki kwa kutekeleza uzazi wa mpango kutokana na uhusiano kati ya umasikini na kasi ya ongezeko la watu.

“Uwekezaji katika wauguzi ni uwekezaji katika uchumi wetu. Kazi yao ni kumsaidia mtu, mgonjwa au mzima, katika kufanya shughuli zinazochangia afya au kupona, ambazo angeweza kufanya bila kusaidiwa kama angekuwa na nguvu, utashi au maarifa ya kutosha,” imeelezwa.

Kafulila amesema changamoto ni nyingi lakini lipo tumaini kadiri nchi inavyojenga na kufungua uchumi, kwani upo uhusiano mkubwa kati ya ukubwa wa uchumi na ubora wa maisha ya wauguzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button