Madaktari taaluma ya Rheumatology wahitajika zaidi

DAR ES SALAAM: Wataalamu wa afya wamewataka wanafunzi wa udaktari na madaktari wa watoto kujikita katika taaluma ya Rheumatology kwa watoto ili kupunguza uhaba mkubwa wa wataalamu wa magonjwa hayo nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Licha ya ongezeko la magonjwa hayo, takwimu zinaonyesha kuwa Afrika yenye zaidi ya watu bilioni 1.4 ina chini ya wataalamu 20 wa Rheumatology kwa watoto, huku Tanzania ikiwa na mtaalamu mmoja pekee katika eneo hilo, hali ambayo imeelezwa kuwa ya kutisha kwa watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya kingamwili na ya viungo.

Tafiti za kimataifa zinaonyesha kuwa magonjwa ya Rheumatology, ambayo ni miongoni mwa magonjwa adimu, huathiri watoto kati ya mmoja hadi wanne kati ya kila watoto 1,000 duniani.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 6 la PAFLAR lililofanyika kwa njia ya kawaida na mtandao, Profesa Francis Furia wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) alisema uhaba wa wataalamu hao umesababisha watoto wengi kuchelewa kugundulika na hivyo kushindwa kupata matibabu kwa wakati.

Profesa Furia ambaye ni daktari bingwa wa watoto alisema kuongeza idadi ya wataalamu wa Rheumatology kwa watoto kutasaidia kuimarisha huduma za afya kwa watoto na kuokoa maisha ya wagonjwa wengi wanaokabiliwa na magonjwa hayo.

“Kutokana na changamoto hizi, tunaendelea kusisitiza umuhimu wa kuongeza wataalamu katika eneo hili. Kupitia kongamano hili la sita, tumetoa mafunzo kwa madaktari wanaobobea na madaktari wa watoto ili waweze kutambua dalili mapema na kutoa tiba kwa wakati,” alisema Profesa Furia.
Pia aliipongeza Serikali kwa hatua ilizochukua kuimarisha huduma hizo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Tanzania imeanza kupiga hatua. Uwekezaji mkubwa umefanyika Muhimbili ambapo huduma hizi sasa zinapatikana. Maabara zimeboreshwa na vipimo vingi vilivyokuwa vikifanyika nje ya nchi sasa vinafanyika hapa nchini,” alisema.
Aliongeza kuwa hospitali hiyo imeanzisha kliniki maalumu kwa watoto wenye magonjwa hayo ambapo zaidi ya watoto 50 kutoka maeneo mbalimbali nchini wanapatiwa matibabu.

“Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha watoto hawa wanapata huduma wanazostahili,” aliongeza.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika ufunguzi wa kongamano hilo, Dk Gunini Kamba alisema Serikali iko tayari kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa fursa za masomo ikiwemo ufadhili kwa taaluma adimu za kitabibu.
“Tunahimiza wote wenye uwezo na nia kujitokeza kusomea taaluma hizi maalumu ili kusaidia kuboresha huduma za afya nchini,” alisema.
Rais wa Jumuiya ya Madaktari wa Watoto ya African League against Rheumatism (PAFLAR), Dk Ayodele Faleye aliwataka viongozi wa serikali barani Afrika kusaidia kufadhili madaktari wa watoto wanaopenda kujifunza taaluma ya Rheumatology kwa watoto.
“Kuna uhitaji mkubwa wa kuongeza wataalamu katika eneo hili,” alisema.
Aidha, alisema kuna haja ya kuimarisha maabara kwani katika nchi nyingi za Afrika sampuli za damu bado hutumwa nje ya bara hilo kwa ajili ya uchunguzi jambo linalochelewesha majibu ya vipimo na matibabu.
“Majibu yanaweza kuchukua siku saba hadi 10 za kazi kurejea, hali inayochelewesha uchunguzi na kuanza kwa matibabu,” alisema.
Aliongeza kuwa kuimarisha uwezo wa maabara za ndani kutasaidia wagonjwa kugundulika mapema na kupata tiba kwa wakati.
Kuhusu dawa, Dk Faleye alisema upatikanaji wake bado ni changamoto kubwa kwa kuwa nyingi zinaagizwa kutoka nje ya Afrika na hivyo kuwa ghali au kutopatikana wakati mwingine.
“Serikali zinapaswa kuingilia kati kuhakikisha dawa hizi zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu,” alisema.



