Bodi ya kahawa kuzalisha miche milioni 30 mwaka 2026/2027

KAGERA: Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kwa kushirikiana na taasisi za utafiti, wadau binafsi, inalenga kuongeza kiwango cha uzalishaji wa miche bora ya kahawa kutoka milioni 20 inayozalishwa kwa sasa hadi milioni 30 kwa mwaka wa fedha 202/2027 ili kukidhi mahitaji ya wakulima.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Aurelia Kamzora ameyasema hayo mkoani Kagera wakati wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi TCB walipowatembelea wakulima wa kahawa, wazalishaji na waandaaji wa vitalu vya miche ya kahawa viwanda vya kuchakata kahawa.

Amesema baada ya Serikali kupandisha bei ya zao la kahawa kwa njia ya mnada sasa kilio kikubwa ni upatikanaji wa Miche ambapo amehaidi miche bora ambayo itaendana na mabadiliko ya tabianchi
Katika ziara hiyo ametoa wito kwa vikundi vya vijana Kuiona fursa iliyopo katika kuandaa vitalu vya kuzalisha miche ya kahawa kwani serikali kupitia TCB imekuwa ikitoa pesa kwa wazalisha wa miche ya kahawa na hiyo ni njia nzuri ya kujipatia kipato kupitia uandaaji wa vitalu.

Mkurugenzi wa TCB, Primus Kmaryo amesema uwepo wa vitalu vya uzalishaji wa miche ni ishara ya uwekezaji wa kesho wa kahawa na miche bora ndiyo msingi wa uzalishaji mkubwa, ambao utaongeza ubora wa kahawa, na kuongeza kipato cha mkulima.

Amesema matamanio ya bodi ni kuona Kagera ikirejea kuwa kinara wa uzalishaji wa kahawa kupitia,matumizi ya miche bora,kuongeza tija kwa ekari, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na kuwavutia vijana kuingia kwenye kilimo cha kahawa.

“Tunawapongeza wataalamu na wakulima wanaosimamia vitalu,wanaounga mnyororo wote wa thamani katika zao la kahawa kwa kazi nzuri wanayofanya,Serikali na wadau wa sekta ya kahawa wataendelea kushirikiana kuhakikisha wakulima wanapata miche bora kwa wakati na kwa wingi zaidi,” amesema Kimaryo.



