Kafulila: Ongezeko la watu changamoto Dira 2050

DAR ES SALAAM: Mkurugenzi Mkuu wa Kituo Cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi David Kafulila amesema changamoto ya uzazi wa mpango ndiyo kikwazo kikubwa cha kiuchumi kinachowakabili familia nyingi nchini, na kuathiri uwezo wa taifa kujenga rasilimali watu bora kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050.
Amesema hayo kupitia mitandao yake ya kijamii ikiwa leo ni maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, mtaalamu mmoja amesema familia ni taasisi ya msingi katika ujenzi wa nchi, uchumi na taifa lolote.
Hata hivyo, ukubwa wa familia unaozidi uwezo wa wazazi kumudu gharama za malezi unawafanya watoto kushindwa kupata elimu, afya na maarifa ya kutosha, na hatimaye kutegemea Serikali kwa kiasi kikubwa.
Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania inakua kwa kasi ya zaidi ya asilimia 3 kwa mwaka, kiwango kilicho juu ya wastani wa Bara la Afrika unaosimama asilimia 2, na wastani wa dunia ambao ni asilimia 1. Kwa sasa Tanzania ni nchi ya 20 kwa idadi ya watu duniani.
Endapo kasi hii itaendelea, nchi itakuwa ya 14 duniani ifikapo 2050, na ya 9 duniani ifikapo 2100.
Linganishi zimetolewa na nchi kama China na India. China ilipunguza kasi ya uzazi kupitia sera ya mtoto mmoja mwaka 1979/1980, na leo hii ina ongezeko hasi la watu, jambo lililochangia kasi yake ya ukuaji wa uchumi kuwa ya pili duniani.
India, ingawa inaongoza kwa idadi ya watu, ina pato la mtu mmoja la chini ya dola 3,000 na ipo nafasi ya 141 duniani, tofauti na Uingereza yenye pato la zaidi ya dola 57,000 kwa mtu mmoja.
Kwa Tanzania, lengo ni kufikia uchumi wa dola trilioni 1 ifikapo 2050. Lakini kwa kasi ya sasa ya ongezeko la watu, nchi itakuwa na watu takriban milioni 137 mwaka 2050, na hivyo pato la mtu mmoja litabaki dola 7,000 pekee. Hii itaiweka Tanzania nafasi ya 100 duniani kwa kipato cha mtu, ingawa kiuchumi itakuwa nafasi ya 35-45.
Ikiwa uchumi utaendelea kukua kwa asilimia 6 kwa mwaka bila kupungua kasi ya ongezeko la watu, uchumi utafikia dola bilioni 380 mwaka 2050, lakini kipato cha mtu kitakuwa dola 2,770 tu, na nchi itakuwa miongoni mwa nchi 30 za mwisho duniani kwa kipato cha mtu.
Ripoti ya Hali ya Umasikini na Maendeleo ya mwaka 2014 ilibainisha kuwa ili Tanzania ifikie Dira 2025 katika sekta ya elimu, ilitakiwa kuajiri walimu 900,000 kati ya 2015 na 2025, sawa na walimu 90,000 kila mwaka. Hii inaonesha jinsi ongezeko kubwa la watu linavyochelewesha maendeleo.
Aidha amesema ili kujenga uchumi mkubwa unaoweza kugharamia afya na elimu bora, Tanzania inahitaji familia ndogo zenye watoto wenye maadili, bidii, afya na maarifa. Kundi hili la watoto wenye umri wa miaka 15 na chini leo, litakuwa nguvu kazi kuu yenye umri wa miaka 24 hadi 39 mwaka 2050.
Amesema kuwa mafanikio hayapatikani kwa kodi na mikopo pekee, bali yanahitaji ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kupitia mfumo wa PPP ili kubeba mzigo wa uwekezaji katika rasilimali watu.



