Serikali yazungumzia hatua kuimarisha biashara kikanda

DODOMA; Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema serikali imeendelea kuchukua hatua za kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kiushuru (NTBs) kati ya Tanzania na nchi jirani, hususan Kenya na Zambia, kwa lengo la kuimarisha biashara na ushirikiano wa kikanda.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Kapinga amesema wizara imeendelea kuratibu majadiliano ya masuala ya biashara na kuondoa vikwazo hivyo kupitia majukwaa mbalimbali ya kikanda.
Ameeleza kuwa kati ya Tanzania na Kenya, wizara imefanikiwa kuendelea kutatua changamoto za kibiashara kupitia mkutano wa Kamati ya Pamoja ya Biashara (JTC) uliofanyika kuanzia Septemba hadi Oktoba 2025 katika jiji la Dar es Salaam.
Amesema katika mkutano huo jumla ya vikwazo 14 vya biashara vilijadiliwa, ambapo sita vilihusu malalamiko yaliyowasilishwa na Tanzania huku vikwazo vinane vikiwasilishwa na Kenya.
“Kati ya vikwazo hivyo 14, vikwazo vitatu vilitatuliwa. Vikwazo hivyo vilihusu ushuru wa bidhaa usio wa haki pamoja na tozo kubwa za stampu kwenye bia za Tanzania zinapouzwa nchini Kenya,” amesema Kapinga.
–
Amesema changamoto zilizokuwa zikikabili usafirishaji wa mbegu kutoka Kenya kuingia Tanzania pamoja na tofauti za gharama za matumizi ya barabara kati ya nchi hizo mbili pia zimepatiwa ufumbuzi.



