Rais Samia kuzingua programu ya mazingira Dodoma

ARUSHA: Rais wa Dk Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Programu ya Kitaifa ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania jijini Dodoma katika kilele cha siku ya Mazingira Duniani Juni 5, 2026.
Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo Kitaifa yatafanyika katika Mkoa wa Dodoma mnamo Juni 5, 2026, ambapo Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atakuwa Mgeni Rasmi.
Akizungumza katika uzinduzi wa usafi wa Mazingira kuelekea siku hiyo ya mazingira Duniani, Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Masauni alisema Rais Dk Samia Suluhu Hassan atakuwa Mgeni Rasmi na atazindua Programu ya Kitaifa ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania.

Alisema Programu hiyo inalenga kutekeleza Dira, 2050 hususan nguzo ya tatu kuhusu Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi ikiwa na lengo la kupanda miti hadi Sh bilioni 2 kwa mwaka, kuimarisha biashara ya Kaboni, Uanzishaji wa Bustani za Kijani katika Miji na shughuli zingine za Kijani.
“Pia inatarajia kuongeza ajira za kijani zinazoweza kufikia zaidi ya elfu ishirini na tano (25,000) ifikapo 2030 kupitia sekta za taka, misitu, kaboni na nishati safi,”alisema.

Alifafanua kuwa tukio hilo ni sehemu ya juhudi za Kitaifa na Kimataifa za kulinda mazingira, kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga jamii yenye afya na ustahimilivu.
Aliongeza Programu hiyo inalenga kutekeleza Dira, 2050 hususan nguzo ya tatu kuhusu Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi ikiwa na lengo la kupanda miti hadi bilioni 2 kwa mwaka, kuimarisha biashara ya Kaboni, Uanzishaji wa Bustani za Kijani katika Miji na shughuli zingine za Kijani. Sambamba na hilo, programu hii inatarajia kuongeza ajira za kijani zinazoweza kufikia zaidi ya elfu ishirini na tano (25,000) ifikapo 2030 kupitia sekta za taka, misitu, kaboni na nishati safi.

Aidha,alileza Dira, 2050 imeweka maono ya Taifa kuwa hadi kufikia mwaka 2050 Tanzania iwe kinara katika matumizi endelevu ya rasilimali, Taifa linalotumia taka kama malighafi kwa manufaa ya kiuchumi na Taifa kinara katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha ustahimilivu na uendelevu wa mazingira.
“Juhudi zinahitajika ili kutekeleza shughuli za mazingira kwa njia jumuishi inayohusisha makundi yote ya kijamii bila kujali jinsia au umri. Kwa jiji la Arusha, tafiti za mwaka 2020 zinaonesha kuwa jiji linazalisha takribani tani 550 za taka ngumu kwa siku, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya taka hizo zinaweza kurejelezwa ikiwa zitadhibitiwa vizuri kupitia uchumi rejeshi,”aliongeza.
“Kwa ngazi ya Kitaifa, Tanzania inakadiriwa kupoteza takribani hekta 469,420 za misitu kila mwaka kutokana na shughuli mbalimbali zisizo endelevu ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa ya kuni na mkaa, kilimo kisicho endelevu, ufugaji holela pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu zinazosababisha uharibifu wa mazingira hali inayochangia kuongezeka kwa gesi joto, kuharibu vyanzo vya maji na kuhatarisha usalama wa bioanuwai,”.
Alieleza Upandaji wa miti yenye matumizi mbalimbali una mchango mkubwa katika kufyonza gesi ya kaboni, kupunguza mmomonyoko wa udongo, kuhifadhi vyanzo vya maji, kutoa matunda pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi kupitia bishara ya Kaboni na kuongeza ustahimilivu dhidi ya athari za Mabadiliko ya Tabianchi.
“Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni hatua muhimu katika kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao umeendelea kuwa miongoni mwa sababu kuu za uharibifu wa misitu nchini. Kuimarisha upatikanaji na matumizi ya nishati safi kama vile gesi asilia, umeme, biogas na teknolojia bora za kupikia kutasaidia kupunguza kasi ya ukataji miti, kupunguza uzalishaji wa gesi joto na kuboresha afya za wananchi hususan wanawake na watoto ambao huathirika zaidi na moshi unaotokana na matumizi ya nishati isiyosafi,” alisisitiza.
Naye Mkuu wa Wilaya Arusha Joseph Mkude alisema ila mmoja ana wajibu wa kutunza kuufadhi mazingira na kuzingatia matumizi ya nishati safi ya kupikia na kusema wote wahimizwa na taasisi nyingi zinatekeleza.



