Teknolojia ufugaji nyuki yaongeza ushiriki wa wanawake

TABORA: WANANCHI na wajasirimali wakiwemo wanawake kutoka katika vikundi vya ufugaji nyuki wilaya za  Sikonge , Urambo na Kaliua mkoani Tabora wamejengewa mazingira bora ya ufugaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa baada ya kujengwa vizimba (mabanda ) vya kuweka mizinga badala ya njia za asili ya utundikaji juu ya miti.

Matumizi hayo yametikana na utekelezaji wa Mradi wa Umimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame unaosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS),kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa ufadhili wa Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wilayani Sikonge wamesema kuwa mradi huo  licha ya kuleta manufaa makubwa pia umewajengea uwezo hususani wanawake kushiriki kikamilifu ufugaji wa nyuki.

Kikundi cha miombo cha wafugaji nyuki kutoka, kijiji na Kata ya Misheni, Wilaya ya Sikonge, kupitia katibu wake, Sarah Mgombozi amesema sasa hivi wanawake wanajua shughuli ya ufugaji nyuki bandani (kizimba).

“Mradi huu uneleta manufaa na hasa kwa wanawake wanahamasika kushiriki kwenye ujasiriamali wa ufugaji wa nyuki,”amesema Mgombozi.

Mgombozi amesema elimu waliyopewa imeleta mabadiliko ya kitaalamu kwa kutumia mizinga ya kisasa na si ya kienyeji na kuchakata kwa kutumia vifaa vya kisasa.

Naye, Mjumbe wa kikundi hicho, Mary Saimon ameshukuru kuanzishwa kwa mradi huo uliowaletea wanawake ufugaji wa kisasa nyuki na umewatoa kwenye adha waliyokuwa wakiipata hapo awali.

“Tumejifunza mengi na hivi sasa chini ya kikundi chetu tutaweza kusomesha watoto, na kuongeza bidii ya kutengeneza mizinga ya kisasa na imekuwa rahisi kwenu wanawake kutundika mizinga na kulina asali,” amesema Mary.

Naye, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS), Hussein Msuya, ambaye pia ni Meneja wa Rasilimali za Nyuki  amesema Mradi huo unalenga kuhifadhi maeneo ya miombo kwa ajili ya kusaidia wananchi waoishi maeneo ya wilaya ya Kaliua, Sikonge na Urambo katika mkoa wa Tabora.

“Tumetembelea eneo la mradi ambapo tumeona kazi ambazo zimefanywa , mradi umejenga kibanda cha kutundika mizinga kwa ajili ya kuwasaidia akina mama kuweza kushiriki kwenye program ya Miombo,” amesema Msuya.

Msuya amesema mradi huo unawasaidia wanawake kuwa na  mazingira rafiki ya ufugaji nyuki  badala ya sasa utundikwa juu ya miti , kitu ambao ni kigumu kwa wanawake kushiriki ufugaji nyuki.

Amesema kuwa kupitia mradi wa Miombo umeweza kujenga bee gages (vibanda nyuki) vipatavyo nane  katika maeneo ya wilaza hizo ambavyo  zinatumika kwenye ufugaji nyuki.

Msuya amesema mradi pia utajenga vituo vya viwanda vya kuchakata asali katika wilaya ya Kaliua na Urambo ambapo kimoja imeshakamilika na kingine kipo hatua za kuanza ujenzi na kuwapa wananchi elimu ya ufugaji wa nyuki .

“ Katika maelezo yao ,wanaeleza kuwa mzinga mmoja wanaweza kupata kilo zaidi ya 29 au 30 na haya ni mafanikio kupitia elimu inayotolewa kupitia mradi Miombo, wameonesha tija tofauti na kabla ya mradi kuwafikia “ amesema Msuya.

Msuya amesema mradi  utajenga vituo vya mbegu za Miombo kwa lengo la kuhifadhi miombo ili kuhakikisha uoto wa miombo unahifadhiwa kupitia  kituo cha kuhifadhia mbegu katika uwanda wa ardhi ya Kaliua.

Kwa upande wake Mwakilishi Msaidizi wa FAO nchini, Charles Tulahi amesema Shirika hilo linatekeleza mradi wa Miombo katika wilaya ya Mlele ya mkoa wa Katavi pamoja na Kaliua , Sikonge na Urambo  za mkoa wa Tabora ili kuzuia uharibifu wa msitu uliojitokeza .

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button