Mwenge wa Uhuru kupitia miradi ya bil 107/- Iringa

IRINGA: Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ametangaza rasmi ujio wa Mwenge wa Uhuru mkoani Iringa kwa mwaka 2026, akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuupokea na kuushangilia mwenge huo unaobeba ujumbe wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Iringa, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mwenge wa Uhuru utawasili mkoani Iringa kesho Mei 26, 2026 ukitokea mkoani Njombe, ambapo mapokezi rasmi yatafanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari Malangali, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kuanzia saa 12:00 asubuhi.

Amesema baada ya mapokezi hayo, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika halmashauri zote tano za Mkoa wa Iringa kwa muda wa siku tano, ukikagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

“Kupitia Mwenge wa Uhuru, tunapata fursa ya kuonesha maendeleo tuliyoyapata lakini pia kurekebisha pale panapohitaji maboresho. Huu ni mwanga wa uwajibikaji na uwazi katika utekelezaji wa miradi ya umma,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mwenge wa Uhuru 2026 mkoani Iringa utapitia jumla ya miradi 39 na kukagua shughuli 25 zinazohusiana na mapambano dhidi ya dawa za kulevya, malaria, UKIMWI, rushwa pamoja na lishe.

Miradi hiyo ina thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 107.5, ambapo imefadhiliwa kwa ushirikiano wa Serikali Kuu, halmashauri, wananchi pamoja na wadau wa maendeleo.

Kheri James amefafanua kuwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2026 ni Wazo Michael Mwang’onda, ambaye atakwenda kuhamasisha ujumbe wa kitaifa wa amani, umoja na mshikamano katika maeneo yote atakayopita.

Katika ratiba hiyo, Mwenge wa Uhuru utapokelewa katika Halmashauri ya Mufindi, Mafinga, Kilolo, Manispaa ya Iringa na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ambapo kila eneo litakuwa na mikutano ya hadhara na mikesha ya amani na furaha.

Aidha, Mwenge huo unatarajiwa kupita katika njia yenye urefu wa zaidi ya kilomita 623.8 ndani ya Mkoa wa Iringa, hatua inayoonesha ukubwa wa ushiriki wa wananchi na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi wa Iringa kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru, kushiriki katika shughuli za maendeleo na kudumisha amani wakati wote wa ziara hiyo.

“Huu ni wakati wa kuonesha mshikamano wetu kama Wairinga na Watanzania kwa ujumla. Tushiriki kikamilifu katika mapokezi, mikutano na mikesha ya Mwenge wa Uhuru,” amesisitiza.

Mwenge wa Uhuru 2026 unatarajiwa kumaliza ziara yake mkoani Iringa na kukabidhiwa kwa Mkoa wa Dodoma Mei 31, 2026 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button