Kizimbani kwa kuingiza magari bila utaratibu

DAR ES SALAAM: WAFANYABIASHARA watatu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Kinondoni Dar es salaam wakikabiliwa na mashitaka tisa yakihusisha kuingiza magari yenye namba za usajili za Afrika Kusini na kuyatumia nchini bila kufuata taratibu za kiforodha na kusababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya zaidi ya Sh milioni 100.
Washitakiwa hao ni George Kaiza (35), Hosiana Sanga (31) na Hamu Sanga (26), wote wakidaiwa kutoa matamko ya uongo kwa maofisa wa forodha wa TRA katika mipaka ya Tanzania na kuingiza magari yenye usajili wa namba za kigeni na kuyatumia bila kufuata taratibu za kiforodha.
Washitakiwa wote walifikishwa mahakamani hapo Mei 26,2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalila na kusomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali Godfrey Nugu akisaidizana na Rozalia Rutagwerela.
Akiwasomea washitakiwa hati ya mashitaka Wakili Nugu alidai wote watatu wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye jumla ya mashitaka tisa, huku kesi namba 11588 ya mwaka 2026 yenye mashitaka saba inamkabili Kaiza pekee yake.
Katika shitaka la kwanza alidai kuwa Machi 27,2026 katika Mpaka wa Mkenda na Kawale mkoani Ruvuma, Kaiza kwa makusudi alitoa taarifa za uongo kwa maofisa forodha kuingiza gari aina ya Toyota Fortuner lenye usajili wa namba za Afrika Kusini KV 05 WWGP kwa lengo la kujipatia kibali cha muda nchini.
Iliendelea kudaiwa kuwa Februari 25, 2026 Kaiza akiwa katika mpaka wa Sirari mkoani Mara alitoa tamko la uongo kwa maofisa forodha wa TRA la kuingiza gari aina ya Ford lenye namba za usajili za Afrika Kusini GFL 712X kwa lengo la kulaghai na kupatiwa kibali cha muda nchini.
Pia ilidaiwa Machi,2026 Kaiza kwa makusudi aliuza gari aina la Toyota Fortuner ambalo lilikuwa limengizwa kwa muda nchini akiwa anafahamu gari hilo lilikuwa limepewa kibali cha muda kilichotolewa na TRA.
Ilidaiwa kuwa Machi 27,2026 Kaiza akiwa katika mpaka wa Mkenda na Kawale mkoani Ruvuma kwa makusudi alikwepa kulipa ushuru kwa TRA Sh milioni 54.6 wa uingizwaji wa bidhaa ambayo ni gari lenye namba za Afrika kusini kitendo ambacho alikuwa anafahamu ni kinyume cha sheria.
Pia katika shtaka lingine Kaiza akiwa katika mpaka wa Sirari mkoani Mara kwa njia za kilaghai na kipatepli alikwepa ushuru wa Sh milioni 30.2 ambayo ni kodi ya ushuru ya kuingiza bidhaa nchini ambayo ni gari aina ya Toyota Fortuner.
Wakili Nugu alidai kuwa kutokana na kitendo hicho cha kukwepa kodi ya ushuru, Kaiza aliisababishia hasara TRA zaidi ya kiasi cha Sh milioni 84.8.
Baada ya kusomwa kwa maahutaka hayo Hakimu Rugemalila alimuonya Kaiza kuwa hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya Uhujumu Uchumi.
Hata hivyo, Wakili Nugu alidai kuwa upelelezi bado unaendelea na hawana pingamizi ya dhamana, lakini Hakimu Rugemarila aliwataka tarehe ijayo wawe wamekamilisha upelelezi wa kesi hiyo.
Wakati huo huo Wakili Nugu alidai kuwa mashitaka mawili kati ya tisa kama ilivyotajwa hapo awali yanawakabili Hosiana na Hamu.
Ilidaiwa kuwa Januari 25,2026 washitakiwa hao wawili wakiwa eneo la Tunduma Songwe walitoa taarifa za uingizwaji wa biadhaa nchini gari aina ya Toyota Fortuner lenye namba za usajili FH 84 RRGP za Afrika Kusini kwa minajili ya kupatiwa kibali cha muda.
Aliendelea kudai kuwa kwa kufanya hivyo washtakiwa hao waliisababishia TRA hasara ya Sh milioni 35.5 kwa kukwepa kulipa kodi ya ushuru wa forodha kwa kuingiza gari aina ya Toyota Fortuner wote wakifahamu kufanya hivyo ni kinyume na sheria.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Hakimu Rugemarila aliwaelekeza kwamba hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu kesi inayomkabili ni ya Uhujumu Uchumi Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza shauri hilo lakini washitakiwa walielezwa kuwa wanahaki ya kupata dhamana.
Hakimu aliwaeleza kuwa maaharti ya dhamana ni kuwa na wadhamini wawili na walitakiwa kulipa dhamana ya fedha taslimu ambayo ni nusu ya kiasi cha ile gharama ambayo ipo kwenye hati ya mashtaka au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika au uthibitisho kama anamiliki mali.
“Kila mshtakiwa anatakiwa awe na wadhami wawili na kila mmoja ataweka nusu ya fedha hiyo ambayo imegawanywa kwa mbili, kwa hiyo wataweka fedha taslimu Sh milioni 8.8 kwa kila mmoja au hati au uthibitisho wa umiliki wa mali,” alisema Hakimu Rugemalila.
Kesi iliahirishwa hadi Juni 9, 2026 kwa ajili ya kutajwa washtakiwa wote wamerudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.


