Wanafunzi BTI waisifu serikali ujenzi wa bweni

TABORA: WANAFUNZI wakike wa Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki (BTI),Tabora ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuwajengea bweni la kisasa la ghorofa moja ambalo limekuwa ni chachu kubwa ya kuongezeka kwa idadi yao kwenye sekta nyuki nchini.

Wanafunzi, Dorotha Bahati, Mwanahawa Khalfani, Zaida Athumani pamoja na Jesca Kalekwa ambao ni wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni hapo kwa nyakati tofauti walieleza kuwa mabweni yaliyopo ni machache na kujengwa kwa bweni hilo litawezesha wenye sifa za kujiunga na chuo hicho ili kupata maarifa, ujuzi na teknolojia ya nyuki ili wanapohitimu wajiajiri au kuajiriwa.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho, Semu Daud amesema kuwa  bweni jipya la kisasa la ghorofa  moja limejengwa kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) na kugharimu Sh bilioni 2.4 nalinauwezo wa  kuchukua wanafunzi zaidi ya 150 .

Amesema Chuo hicho kilianzishwa mwaka 1949 na wakoloni kwa ajili ya utafiti wa misitu ya miombo na ilipofika mwaka 1978 Serikali ilikibadilisha na kuwa Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki kwa masomo ya ngazi ya Astashahada na Stashahada ya ufugaji nyuki.

“Serikali tangu kipindi hicho imeendelea kukiwezesha na kukiboresha  na kutokana na hayo kwa sasa wanawake wanachukua nafasi kubwa zaidi katika sekta nyuki tofauti na ilivyokuwa zamani” amesema Semu.

Semu amesema chuo hicho kina wanafunzi takribani 350, ambapo asilimia 54 ni wanaume na asilimia 46 ni wanawake huku lengo likiwa kufikia uwiano wa 50 kwa 50.

Amesema kuwa ongezeko hilo limetokana na mwamko mkubwa wa jamii, matumizi ya teknolojia za kisasa za ufugaji nyuki pamoja na jitihada za Serikali na wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta hiyo nchini.

Semu amesema teknolojia mpya zimebadili kabisa mazingira ya kazi yaliyokuwa yakionekana kuwa magumu kwa wanawake, kwani kwa sasa mizinga mingi inatundikwa katika vichanja badala ya miti mirefu, hali iliyorahisisha kazi na kuongeza usalama kwa wafugaji.

Amesema miaka ya nyuma, sekta ya ufugaji nyuki ilionekana kuwa kazi ngumu iliyowafaa zaidi wanaume kutokana na mazingira yake ya kazi, ikiwemo kutundika mizinga juu ya miti na kufanya shughuli katika maeneo ya misitu.

“Taswira hiyo sasa imeanza kubadilika kwa kasi huku wanawake wengi wakijitokeza kujiunga na mafunzo ya ufugaji nyuki nchini katika miaka ya hivi karibuni” amesema Semu.

Semu pia amesema  mafanikio hayo yamechangiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuwa nguzo muhimu katika mageuzi ya sekta ya ufugaji nyuki kupitia uwekezaji mkubwa katika mafunzo, miundombinu na programu za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa BTI.

Amesema TFS imekuwa ikitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji chuoni hapo.

Pia TFS inapokea wanafunzi wengi katika vituo mbalimbali kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo yanayowasaidia kuoanisha maarifa ya darasani na mazingira halisi ya kazi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button