CCM yaonya watakaokwamisha huduma kwa wananchi

KILIMANJARO: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitakuwa tayari kuvumilia mtumishi yeyote wa chama au serikali atakayekwamisha jitihada za utoaji huduma kwa wananchi, kikisisitiza kuwa hatua zitachukuliwa bila kuangalia cheo, umaarufu wala umri wa mhusika.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 29,2026 na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi alipotembelea na kukagua mradi wa Maabara katika Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto iliyopo katika Kata ya Ivaeny wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro.

Kihongosi amesema utekelezaji wa Ilani ya CCM lazima uendane na uwajibikaji wa viongozi pamoja na watumishi wa serikali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazostahili.

“Endapo kutakuwa na mambo yatakayokwamisha utekelezaji wa ilani, wananchi watatuhukumu na sisi kama chama hatutakubali. Mtumishi wa chama au wa serikali kwa namna yoyote atakayekwamisha jitihada za serikali katika kupeleka huduma kwa wananchi, tutachukua hatua bila kuangalia umaarufu, umri wala cheo,” amesema Kihongosi.

Amesema kila mmoja anapaswa kusimama kwenye nafasi yake na kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu kwa maslahi ya Watanzania.

Pia amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Nurdin Babu pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo, akisema thamani ya uwekezaji uliofanyika inaonesha wazi fedha za serikali zimesimamiwa kwa uadilifu.

“Ukiangalia majengo yaliyojengwa na thamani ya fedha iliyoletwa hapa, unaona kabisa kulikuwa na watu waadilifu waliosimamia fedha za serikali,” amesema.

Pia ameipongeza menejimenti ya Hospitali ya Kibong’oto, madaktari, manesi na wataalamu wa afya kwa kujitolea kutoa huduma kwa wananchi, akisema kazi yao ni ya kipekee na yenye kugusa maisha ya watu wengi.

Alisema CCM imeridhishwa na utekelezaji wa Ilani katika sekta ya afya mkoani humo, huku akibainisha kuwa huduma bora zinazotolewa zinaendelea kuongeza imani ya wananchi kwa serikali na chama hicho.

Awali, Meneja wa Maabara ya Afya ya Jamii katika Hospitali ya Kibong’oto, Shaban Mziray alisema maabara hiyo imegharu jumla ya kiasi cha Sh bilioni 22.5 katika utekelezaji wake ikijumuisha ujenzi wa jengo na vifaa vyake.

Alisema maabara hiyo ilianza kutumika mwaka 2023 na imekuwa na mchango mkubwa katika ufuatiliaji wa magonjwa ya milipuko, kubaini usugu wa vimelea dhidi ya dawa pamoja na kufanya tafiti mbalimbali za kimkakati.

Alisema maabara hiyo imehusika katika tafiti zilizosaidia kufupisha muda wa matibabu ya kifua kikuu sugu kutoka zaidi ya miezi 20 hadi miezi sita.

Mziray alisema maabara hiyo yenye ukubwa wa nusu hekari ni miongoni mwa maabara kubwa zaidi nchini kwa uwekezaji wake, huku ikiwa na benki ya sampuli yenye uwezo wa kuhifadhi lita 47000 za sampuli kwa muda mrefu kwa ajili ya tafiti, ugunduzi wa chanjo na tiba mbalimbali.

Aliongeza kuwa maabara hiyo pia hufanya uchunguzi wa bakteria, fangasi na vinasaba vya magonjwa mbalimbali pamoja na kuchakata vimelea hatarishi ikiwemo TB sugu zaidi kupitia mfumo wa usalama wa kibiolojia ngazi ya tatu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button