Wanaume waonywa kutelekeza watoto

DODOMA: Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, amewataka wanaume nchini kuacha tabia ya kutelekeza watoto wenye ulemavu na kushiriki kikamilifu katika malezi yao.
Amesisitiza kuwa serikali imeweka mifumo mbalimbali ya kuhakikisha watoto hao wanapata haki na huduma za msingi ili waweze kutimiza ndoto zao.
Ummy alitoa rai hiyo wakati wa ziara yake katika Kituo cha Watoto Wenye Mahitaji Maalum cha Mlali Rehabilitation Center kilichopo wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki.
“Nitumie fursa hii kuwaomba kina baba kote nchini kuwaunga mkono kina mama wanapopata watoto wenye ulemavu mara nyingi mtoto mwenye ulemavu huachwa kuwa jukumu la mama pekee, wakati mtoto asiye na ulemavu huonekana kuwa wa baba, hii siyo sahihi,” alisema Ummy.

Aliongeza kuwa watoto wenye ulemavu wanahitaji upendo, malezi na ushirikiano wa wazazi wote wawili ili waweze kukua katika mazingira bora na yenye amani.
“Naomba kina baba msiwakimbie watoto wenye ulemavu wala kuwaacha kina mama wakibeba mzigo huo peke yao, tuishi kwa upendo na mshikamano katika familia zetu,” alisisitiza.

Aidha, Naibu Waziri huyo alieleza kuwa watoto wenye ulemavu wanaokaa mitaani au katika mazingira hatarishi mara nyingi hukumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji, hivyo akaitaka jamii kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi vitendo hivyo vinapotokea.
“Watoto wenye ulemavu wanastahili kulindwa kama watoto wengine. Endapo watafanyiwa ukatili au unyanyasaji, jamii na familia zitoe taarifa kwa mamlaka husika ili hatua za kisheria zichukuliwe,” alisema.
Kwa upande wao, baadhi ya wanawake ambao watoto wao wanapata huduma katika kituo hicho walikiri kutelekezwa na wenza wao mara baada ya kujifungua watoto wenye ulemavu, huku wakieleza kuwa huduma zinazotolewa katika kituo hicho zimechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha afya na maendeleo ya watoto wao.
Mmoja wa wazazi hao, Suzana, alisema mtoto wake alipofikishwa kituoni hapo alikuwa hawezi kukaa wala kushikilia shingo vizuri, lakini hali yake imeimarika baada ya kupata huduma za tiba na uangalizi.

“Ninawashauri kina mama tusikate tamaa. Tuendelee kuwalea watoto wetu kwa moyo wa kujitolea, namshukuru Mungu na kituo hiki kwa sababu mwanangu sasa anaendelea vizuri tofauti na awali,” alisema.
Ziara hiyo ya Naibu Waziri iliambatana na utoaji wa msaada wa bidhaa mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho, ikiwemo sukari, sabuni, maharage, viazi, mafuta ya kupikia na mchele.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Mlali Rehabilitation Center umeiomba Serikali kusamehe deni la kodi ya ardhi linalofikia zaidi ya Sh milioni 9, ukieleza kuwa kituo hicho kinatoa huduma za kijamii kwa watoto wenye mahitaji maalum na hakifanyi shughuli za kibiashara kwa ajili ya kupata faida.



