CCM yahitimisha kampeni Isimani, Chatanda atoa ahadi

IRINGA: Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimehitimisha kampeni zake za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Isimani kwa mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Migoli, huku viongozi wa chama wakionesha imani kubwa ya ushindi na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa mgombea wake, Emanuela Mtatifikolo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Taifa, Mary Chatanda, mmoja wa viongozi wa chama katika kuhitimisha kampeni hizo, alisema CCM imefanya kazi kubwa ya kuzungumza na wananchi katika vijiji vyote vya jimbo hilo na kwamba hakuna sababu ya chama hicho kushindwa uchaguzi huo.

“Hakuna kura itakayopotea Isimani. Tutakiheshimisha chama chetu kwa kumchagua Emanuela. Wanawake kesho waamsheni waume zenu mapema kwenda kupiga kura. Kama mmegombana nao leo waambieni ‘hello baby’, msikasirikiane leo ili kesho wakapige kura,” alisema Chatanda huku akipata shangwe na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo.
Katika hali iliyogusa hisia za wananchi, Mbunge wa Viti Maalum, Fatma Rembo, alipiga magoti mbele ya wananchi akiwaomba kumpigia kura mgombea huyo wa CCM, akisema wanawake katika vyombo vya maamuzi ni muhimu katika kusukuma mbele agenda za maendeleo na ustawi wa wanawake.
“Tunapopata wanawake wengi katika nafasi za uamuzi, tunapata sauti kubwa zaidi ya kutetea maendeleo ya wanawake, watoto na familia kwa ujumla,” alisema Rembo.

Mratibu wa Kampeni za CCM Jimbo la Isimani, Solo Kasaba, alisema chama hicho kimefanya kampeni za kina katika jimbo lote, hali inayowapa uhakika wa ushindi.
“Tumefanya kampeni katika kata zote 13, tumefika vijiji vyote 60 na kufanya mikutano 84. Tumewafikia wananchi wa kila kona ya Isimani na tumeeleza sera zetu kwa kina,” alisema Kasaba.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa, Constantino Kiwele, alisema mgombea huyo amewafikia wananchi wa makundi yote muhimu ya kijamii na kiuchumi.
“Mgombea anajiuza mwenyewe. Tumewafikia wazee, vijana, wanawake, bodaboda, mama lishe na makundi mengine yote. Wananchi wameelewa agenda zetu na wana matumaini makubwa na CCM,” alisema.
Mbunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga, alitumia mkutano huo kueleza mafanikio ya maendeleo yaliyofikiwa Isimani chini ya Serikali ya CCM, akitaja uwepo wa vituo vya afya 13 pamoja na mradi mkubwa wa umwagiliaji wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 54.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa alisema wananchi wa Isimani wameendelea kuonyesha imani kubwa kwa CCM kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha yao moja kwa moja.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas, alimpongeza Mary Chatanda kwa namna alivyojitolea kuzunguka vijiji vyote vya Isimani wakati wa kampeni.

“Tunamshukuru sana Mama Chatanda. Amefanya kazi kubwa kiasi kwamba ungeweza kudhani yeye ndiye mgombea wa uchaguzi huu,” alisema Asas.
Akizungumza kama mgeni rasmi wa mkutano huo, Katibu wa NEC, Idara ya Oganaizesheni wa CCM, Issa Haji Ussi maarufu kama Gavu, alisema uchaguzi wa Emanuela utatoa kasi mpya ya maendeleo katika jimbo hilo, hususan kwenye sekta za umeme, kilimo, mifugo na maji.
Alisema serikali ina mpango wa kuhakikisha kila kijiji na vitongoji vyake vinapata huduma ya umeme ili kuongeza uzalishaji na kuinua vipato vya wananchi.
“Tunataka kila kaya iwe na umeme kwa matumizi ya nyumbani na shughuli za kiuchumi. Mtu wa kuyasimamia maendeleo ya Isimani ni Emanuela. Hii ndiyo njia ya kuendelea kuwaondoa wananchi kwenye dimbwi la umasikini,” alisema Gavu.
Alisema serikali inaendelea kuwekeza katika maeneo ya uzalishaji kwa kuanzisha viwanda vidogo vinavyoongeza thamani ya mazao na mazao ya mifugo ili kuhakikisha wakulima na wafugaji wanapata masoko ya uhakika.

Aidha alisema baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa umwagiliaji wa Isimani, serikali imepanga kuanzisha miradi mingine miwili ya umwagiliaji ili kuongeza fursa za uzalishaji, ajira na uwekezaji.
Katika sekta ya mifugo, alisema serikali inalenga kuongeza maeneo ya malisho, kujenga majosho na visima vya maji kwa ajili ya mifugo ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
“Maji safi na salama yatafika Isimani. Mkimchagua Emanuela mtakuwa mmeendeleza fikra nzuri na maono ya maendeleo yaliyoachwa na mtangulizi wake,” alisema.

Akihitimisha mkutano huo, mgombea wa CCM, Emanuela Mtatifikolo, alisema amepata nafasi ya kuzungumza na wananchi katika vijiji vyote vya Isimani na kusikiliza changamoto zao, huku akiahidi kuzitekeleza kwa kasi kubwa mara baada ya kuchaguliwa.
“Nimezungumza na wananchi katika vijiji vyote. Yale yote tuliyoyaahidi tunakwenda kuyatekeleza kwa kasi ile ile kwa sababu chama kipo na serikali ya CCM ipo,” alisema.
Akirejea urithi wa maendeleo ulioachwa na aliyekuwa Mbunge wa Isimani, William Lukuvi, Emanuela alisema yuko tayari kuendeleza kasi hiyo ya maendeleo.
“Viatu vya Lukuvi vinanitosha, havinipwi wala kunibana. Wananchi wa Isimani wajiandae kwa kasi kubwa zaidi ya maendeleo,” alisema huku akimaliza kampeni zake kwa ahadi ya kusimamia kwa nguvu utekelezaji wa miradi ya maji, umeme, afya, kilimo na mifugo katika jimbo hilo.



